WASHINGTON, MAREKANI

BAADA ya wiki kadhaa za kuapa kwamba atashinda vita vya kubakia madarakani, Rais wa Marekani Donald Trump hatimaye ameonekana kuanza kukiri, japo si moja kwa moja, kushindwa na Joe Biden katika uchaguzi uliopita.

Katika ujumbe wa video alioutoa hapo Trump alisema ni sharti utawala wake ukumbukwe kwa kile ulichokifanya.

Trump aliutoa ujumbe huo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kurudi mapema mjini Washington kutoka likizo kwenye hoteli yake iliyoko mjini Florida.

Aliyasema hayo wakati ambapo kuna mapambano kati yake na bunge la Congress kuhusiana na mswada wa ulinzi na malipo ya misaada wanayopokea Wamarekani kutokana na athari za kiuchumi za virusi vya corona.

Trump alisifu mafanikio ya utawala wake ambao alisema ulifanikiwa katika kupambana na janga la virusi vya corona na kuukuza upya uchumi wa nchi hiyo.

Seneta wa Republican Josh Hawley alisema atapinga kushinda kwa Joe Biden wiki ijayo bunge la Congress litakapokutana.