TUNAKUBALIANA kabisa na wale waliosema elimu ni hazina. Maneno haya yenye hekima tunataka kuyanasibisha na matatizo mengi yanayotokea hasa katika suala zima la upotevu wa rasilimali asili muhimu duniani.

Upotevu wa vyanzo vya maji, hili ni tatizo linaloikabili dunia kwa sasa ambalo linatokana na sababu kadhaa zikiwemo zinazoababishwa na mikono ya mwanadam.

Kipawa cha mwanadamu katika suala zima la ubunifu kimeongezeka maradufu hasa katika dunia ya sasa ya teknolojia. Wanaweza kubuni zana za kimaendeleo lakini zinazoleta athari kwa watu na mazingira.

Wakati mwengine uvumbuzi huo hauzingatii athari hizo ila hufanywa kwa kukidhi matwaka ya teknolojia ambayo hubadilika kila baada ya muda mfupi.

Kwa upande wa teknolojia, kwa mfano zipo zana nyepesi tu ambazo hutumia kuharibu mazingira kama vile misumeno ya moto kwa ajili ya kukatia miti bila mpango maalum.

Katika kutimiza mahitaji ya watu yanayokua kwa kasi. Ukataji wa miti kwa mfano, hupunguza kiwango cha hewa safi, miti inanyonya hewa chafu na kutoa hewa safi ambayo tunaihitaji kwa matumizi wetu.

Matokeo yake kiwango cha joto huongezeka na kuharibu mifumo mingine ya hewa. Hali hii huchangia kutokea majanga ya kiasili kama vile mvua kubwa na mafuriko, maporomoko ya udongo au matope, ukame unaosababisha njaa na majanga mengine.

Wakati dunia ilipokuwa mstari wa mbele kuhifadhi mazingira jamii ilishajiika na kampeni ya ‘kata mti panda miti’ wala hakukuwa na malalamiko ya upotevu wa vyanzo maji tunayoyashuhudia sasa.

Wimbo huu ulitekelezwa kwa vitendo na kila mmoja alijua umuhimu wa kuotesha miti. Lakini binadamu tunahitaji kukumbushwa juu ya mambo ambayo ni faida ili kuepusha athari zinaoweza kuwakumba wengine hata wasiohusika.

Haya yanaweza kuleta matokeo ya mabadiliko ya mambo mengi sana ambayo miongoni mwao tukashindwa kuyatekeleza ingawaje mawazo yake yalikuwepo tokea zamani. Ili kupunguza ongezeko la watu duniani watu washajiishwe kufuata kanuni za uzazi salama kurahisisha huduma zao kwa mujibu wa mahitaji yao.

Jengine ni kuwa na mipango ya kujenga nyumba za kisasa zaidi za ghorofa zitakazokidhi kiwango ili badala ya kujenga za chini, zitasaidia kuwa na eneo litakaloweza kutumika kwa kilimo.

Elimu ya kutojenga katika maeneo ya vianzio vya maji nayo pia ni muhimu kwa maisha ya binadamu kwani hali hiyo inaweza kuchangia maafa zaidi pale yanapotokea mafuriko.

Kutokana na teknolojia ya habari na mawasiliano hivi sasa na dunia kukunjwa mfano wa kijiji, wengi wetu tunashuhudia matukio ya kujaa maji kuanzia katika mito na maziwa hali inayoleta athari kubwaa sana.

Hatusemi kuwa kupanda miti kunaweza kuondosha mafuriko lakini athari zake zinaweza kupungua sio sawa na maeneo ambayo hakuna miti kabisa.

Hivyo, jamii inaweza kuleta mabadiliko makubwa juu ya elimu ya mazingira na nyengine zitakazokuwa na uhusiano wa kuhifadhi mazingira kwa maslahi ya wote.

Ushahidi unaonesha kuwa vyombo vinavyohusika vinapokuwa na msimamo wa kuleta mabadiliko na jamii pia huelekea huko, lakini wanaporegeza msimamo jamii nayo pia hukosa msimamizi.

Matokeo yake ni hasara kwa watu wengine na taifa ambapo badala ya kuhudumia taifa la watu wenye siha njema inahudumia watu waliodhofu kwa matatizo ambayo yangeweza kuepukika.