NA MWAJUMA JUMA

KOCHA wa timu ya Simba Suleiman Matola amesema kukosa nafasi ya kucheza kwa baadhi ya wachezaji wake katika mechi isitafsiriwa kuwa hawana uwezo.

Akizungumza mara baada ya mchezo baina ya timu yake na Mtibwa ambapo Simba ilishinda mabao 2-0, alisema Simba ina wachezaji wengi na wote wana uwezo, hivyo kwa wale ambao hawajapangwa haina maana kwamba kiwango chao kimepungua.

Hivyo alichukua fursa hiyo kuwapongeza wachezaji wake kwa kiwango walichokionyesha katika kila mechi.

“Ni kweli timu yetu ina wachezaji karibu wote wenye uwezo na wengine kukosa nafasi, lakini haina maana kuwa wameshuka viwango”, alisema.

Hata hivyo alisema pamoja na wachezaji hao kucheza mechi mbili mfululizo bila ya kupumzika, lakini wamefanya kazi nzuri ambayo iliyowafanya wafikie nusu fainali.

Akizungumzia ratiba ya michuano hiyo alisema walipofahamu kuwa wapo kundi moja na Mtibwa, walijua wana kazi ya kulipa kisasi baada ya fainali ya mwaka jana kuwafunga.

“Wakati tunapata tu ratiba tuligundua kuwa tuna kisasi na lazima tujiandae kwani hatuwezi kufungwa mara mbili”, alisema.

Kwa upande wake kocha wa Mtibwa Vincent Barnabas Saramba alikiri wachezaji wa Simba walikuwa na kiwango bora kulinganisha na wachezaji wake.

Alisema licha ya mwaka jana kutwaa ubingwa lakini msimu huu timu yake imebadilika sana, kwani ina wachezaji wengi kutoka timu B ambao bado wanaendelea kujifunza na kupata uzoefu.

Mtibwa ambao ni mabingwa watetezi katika mchezo huo ilifungwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Miraji Athuman na Hassan Dilunga na kuvuliwa ubingwa.