BADO vijana wetu wanazo fursa nyingi za kujiandaa kuwa wajasiriamali wazuri na kuhodhi soko la ajira katika visiwa vyetu, licha ya kuwepo changamaoto za hapa na pale.

Pamoja na ukweli kwamba ardhi yetu ni ndogo, hatuna nyenzo na zana na vifaa bora vya uvuvi na hata skuli za ufundi kuwa bado hazitoshi, iwapo tutakuwa na mipango na mikakati kabambe changamoto hizo zitaweza kupatiwa ufumbuzi.

Wawekezaji wengi wamefungua miradi ya utalii, lakini hadi sasa tunajiuliza inakuwaje ajira kwenye sekta hiyo wageni wazitawale, wakati tunao vijana wengi wenye nguvu na baadhi yao wamesoma vizuri ambao bila shaka wanaweza kufanikisha kazi vizuri na kuinua vipato vyao na jamii zao.

Miongoni mwa hoja zinazotolewa na watu tafauti wakiwemo wamiliki wa miradi hiyo ni kwamba, vijana wetu wengi hawana sifa zinazohitajika katika ajira nyingi zinazopatikana kwenye miradi hiyo, wengine wanasema vijana wetu wamekuwa na tabia ya kuchagua kazi.

Hili la vijana kukosa sifa nalo si la kupuuzwa na la muhimu kwa sasa ni kuhakikisha tunaandaa mazingira yatakayowafanya vijana wetu wa kike na wa kiume wawe tayari kukabiliana na ushindani katika soko.

Ni vyema ufanyike utambuzi wa fani zipi ambazo wakisoma vijana wetu katika ngazi za juu wataweza kutawala soko la ajira za utalii na hivyo kufikiwa malengo ya kuanzishwa sera ya utalii.

Katika hili hatuna budi kupongeza hatua ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kukiimarisha Chuo cha Hoteli na Utalii, na hadi sasa kukiwezesha kuwa sehmu ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA.

Kiukweli hii ni hatua muafaka itakayowawezesha vijana wetu kufikia malengo ya kunufaika zaidi na sekta ya utalii ambayo kwa sasa ndio nguzo ya uchumi wa Zanzibar.

Mbali na hatua hiyo, pia tutaweza kufikia malengo ya kuzikamata ajira nyingi zaidi kwa kuanzisha sekondari nyingi za ufundi pamoja na vyuo vitakavyotoa mafunzo ya amali (stadi za maisha). Hatua hii itawajengea vijana wetu misingi tangu wanapokuwa katika skuli na vyuo.

Pale wanapohitimu hata kama hawakuajiriwa, lakini watamudu kujiajiri na kuajiri wengine kutokana na utaalamu wao wa ufundi na kazi za mikono walionao.