NA ABDI SHAMNA, IKULU

WAZIRI wa Nchi (OR), Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana na wadau katika kutekeleza mikakati maalum ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji.

Waziri Haroun alisema hayo wakati akifungua tamasha la kwanza la pongezi kwa Wana Sunni Madrasa, lililofanyika kwenye ukumbi wa Sunni Madrasa, Mkunazini jijini Zanzibar na kueleza kuwa mikakati hiyo ni pamoja na uliopangwa kutekelezwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2017 – 2022.

Akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Haroun aliahidi kukutana na wadau wanaoshughulikia vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo jeshi la polisi, mahakama na ofisi ya Muendesha Mashtaka kwa lengo la kujenga mikakati ili kuharakisha usikilizaji wa kesi za makosa hayo yaliyoshamiri nchini.

Alisema serikali hairidhishwi na mrundikano uliopo wa kesi za udhalilishaji na hivyo akaitaka jamii kujenga mashirikiano na vyombo vya sheria ili kufanikisha mchakato wa kesi pamoja na kuondokana na muhali.

Aidha waziri huyo aliwapongeza walimu wanaofundisha fani ya ‘Nasheed’ kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwoamba kuendeleza juhudi za kuisambaza taaluma hiyo hadi vijijini Unguja na Pemba.

Katika hafla hiyo Waziri Haroun alikabidhi zawadi kwa washindi wa Tamasha la ‘Nasheed’, ambapo mwanafunzi Nasra Abdalla Mohamed alikuwa mshindi wa kwanza na kuzawadiwa Friji, Mkoba pamoja na Mas-hafu.

Aidha mwanafunzi Asiat Ramadhan Jussa, alikuwa mshindi wa pili na kuzawadiwa zawadi za cherehani, mkoba na mas-hafu, huku mwanafunzi Mudrik Msellem Ali akiondoka na ushindi wa tatu na kuzawadiwa baiskeli, mkoba na Mas-hafu.

Mapema, Katibu Mtendaji, Baraza la Sensa, Sanaa na Filamu (BASFU), Dk. Omar Abdalla Adamu, aliwashukuru waandaaji wa tamasha hilo na kusema wamekamilisha taratibu zote za kisheria na kufuata mila, silka na utamaduni wa Mzanzibari.