NA LAYLAT KHALFAN

MAMLAKA ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar, imedhamiria kuvikagua vyombo na leseni za madereva kwa lengo la kuthibitisha uimara wake kupunguza ajali.

Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mohammed Simba Hassan, alieleza hayo ofisini kwake Mwanakwerekwe wakati akizungumza na mwandishi wa habari wa Zanzibarleo, kuhusiana na zoezi la ukaguzi wa vyombo hivyo linaloendelea.

Alisema zoezi hilo litakwenda kwa awamu katika kipindi hiki na kuanza kuvikagua vyombo vinavyotoa huduma ya usafiri wa umma ikifuatiwa na sekta ya gari za mizigo, gari za binafsi pamoja na vyombo vya magurudumu mawili.

Alisema kwa vile vyombo ambavyo watakavyovigundua na matatizo, wahusika watalazimika kuvirekebisha ili kuhakikisha usalama barabarani unaimarika kwa kiwango kikubwa.

“Tukimaliza ukaguzi huu wa vyombo tutalazimika kuingia kwenye ukaguzi wa leseni pamoja na utambuzi wa leseni za madereva wote,” alisema.

Simba alisema wamebaini katika barabara zao kuna vyombo vingi ambavyo vinatumia nyaraka ambazo si sahihi na zinamepatikana kwa utaratibu ambao haukubaliki, vyengine vinatumia vifaa kwa kuazima katika magari mengine, jambo ambalo si utaratibu.

Alisema licha ya kuwa mamlaka imekuwa ikibaini mambo mengi yanayohusiana na barabara lakini kuna kasoro kubwa ya kutoijua idadi ya vyombo vinavyotembea barabarani.

Alisema kwa siku mamlaka inakua na idadi kubwa ya vyombo vinavyoingia barabarani lakini ukiangalia vyombo hivyo havilingani na ule uhalisia, hivyo mamlaka baada ya kugundua hilo, imeamua kwa makusudi kuvifanyia utafiti vyombo hivyo ili kuweza kupata idadi halisi ya vyombo hivyo.

“Kazi yetu kubwa ni kutoa elimu mara kwa mara ya usalama barabarani kwa wadau wetu kwa kuweza kuwaambia kitu gani kinaweza kufanywa na kitu gani hakiwezi kufanywa kwenye barabara,” alisema.

Alisema suala la ukaguzi ni suala la kisheria, hivyo kwa wale wanaokutwa na makosa makubwa kama vile kufoji nyaraka na mambo mengine yanayofanana na hayo kwa kipindi hichi wanawachukulia hatua ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.