NA MARYAM HASSAN

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Prof. Palamagamba John Kabudi, amekihakikishia kituo cha kutotolea vifanga vya samaki Beit el Ras kuwaletea wataalamu wanaoendana na kazi hizo.

Aliyasema hayo baada ya kufanya ziara katika kituo hicho akiongozana na viongozi mbali mbali akiwemo Waziri wa Uchumi wa Buluu na Maendeleo ya Uvuvi Abdalla Hussein Kombo.

Alisema imefika wakati kwa taasisi zote zinazohusiana na masuala ya uvuvi kuhakikisha kuwa wanashirikiana katika sekta hiyo ili kuleta tija katika kituo hicho.

Alisema wataalamu hao watatoa elimu ya uzalishaji bora wa vifaranga ambavyo watapatiwa wananchi kwa ajili ya kuendeleza ufugaji.

Aidha alisema fursa hiyo pia watawashirikisha mabalozi walio katika nchi za nje kutoa ushirikiano katika kituo hicho.

Aliongeza kuwa katika kutafuta wataalamu hao watahakikisha wanatumia juhudi mbali mbali ili wapatikane mara moja.

Pia alisema pindi watakapofika wataalamu hao elimu hiyo isitolewe kwa watu wachache bali wawakusanye wananchi wenye nia ya kufuga samaki kwa ajili ya kupatiwa elimu hiyo.

Katika ziara yake hiyo Waziri huyo alifurahishwa baada ya kuona kituo hicho kimeanza kuzalisha samaki aina ya Sato.

“Nimefurahi kuona sasa Zanzibar nanyi mmeanza kuzalisha samaki aina ya Sato ambapo kawaida imezoeleka kuwa samaki wa aina hii hupatikana Tanzania bara pekee, hongereni sana kuwa na Sato wa Zanzibar,” alisema.

Sambamba na hayo aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanazalisha samaki wengine ili kupunguza uhaba wa samaki hapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa SMZ na SMT kwa pamoja zitahakikisha kuwa wanakifanya kituo hicho kuwa cha mfano pamoja na kuzalisha vifanga vya samaki vyenye ubora.

Kwa upande wa Naibu Katibu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Maendeleo ya Uvuvi, Omar Ali Ameir alisema awamu ya nane chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, imedhamiria kuimarisha uchumi wa buluu katika bahari kuu.

Alisema wizara yake inakusudia kuongeza kasi ya uzalishaji samaki kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote wa Unguja na Pemba.

Aidha alieleza kuwa bado wanakabiliwa na uhaba wa wataalamu pamoja na ukosefu wa mafunzo ambayo yataleta kasi ya uzalishaji wa vifaranga kwa wingi.

Hivyo alimuomba Waziri huyo kuwatafutia wataalamu kutoka nje ya nchi ambao watatoa elimu ya ufugaji bora wa vifaranga vya samaki.

Mapema Mratibu wa kituo hicho, Burhani Mussa Hassan, alisema licha ya jitihada wanazochukua kituo cha kuzalisha samaki aina ya Mwatiko mpaka sasa hawajafanikiwa.

Alisema mpaka sasa hawajajua wapi wanapokosea lakini aliiomba Wizara husika kubuni mbinu mbadala ili samaki hao wapate kuzalishwa kituoni hapo.