N

NA ABOUD MAHMOUD

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeelezwa kuwa itaendelea kutoa kipaumbele kwa vijana walio tayari kujitolea na kuiletea nchi maendeleo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk. Soud Nahoda Hassan, alipoungana na vijana wa Jumuiya ya Kupambana na Mabadiliko ya Tabia nchi Zanzibar (ZACCA) wakati wa zoezi la upandaji wa miti ya mikoko katika pwani ya Kinazini, mjini Unguja.

 “Ni wajibu wetu Serikali kuwaunga mkono vijana wanaojali uzalendo na kuleta maendeleo katika nchi yetu ili kuondokana na changamoto mbali mbali zinazotukabili,” alisema.

Alisema kitendo kinachofanywa na vijana hao cha kuipenda nchi yao na kumuunga mkono Rais wa Zanzibar bila ya kutarajia malipo ni jambo jema ambalo linahitaji kutiliwa mkazo kwa maslahi ya taifa.

 “Naziomba taasisi mbali mbali nchini kuwasaidia vijana ambao wamekua mstari wa mbele katika kuhakikisha wanailetea nchi maendeleo,”alisema.

Aidha Dk. Nahoda aliipongeza ZACCA kwa ubunifu walioufanya wa kuhifadhi mazingira katika maeneo yanayoweza kuleta athari kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Mali Asili zisizorejesheka, Nassor Mkarafuu, alisema dunia imekabiliwa na tatizo la tabia nchi ambalo chanzo chake ni jamii.

“Mabadiliko ya shughuli za kijamii ndio chanzo cha tatizo hili kwani jamii ndiyo inayokata miti bila ya kutizama athari ambazo zinazoweza kutokea nchini,” alieleza Mkarafuu.

Naye Mwenyekiti wa ZACCA, Mahfoudh Haji, alisema jumuiya yake kupitia programu ya ‘Usafi HUB’ imepanga kutembelea maeneo 30 ya Zanzibar katika upandaji wa miti, uwekeji mazingira safi na kutoa taaluma kwa jamii.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema katika programu hiyo imejipangia kupanda miche ya mikoko 50,000 kwa mwaka na aina nyengine za miti 20,000 kwa Zanzibar nzima.

Jumla ya miche ya mikoko 1,000 imepandwa katika eneo la Kinazini ambapo taasisi mbali mbali zilishiriki ikiwemo Wanahabari Vijana, NEZA, JIKA na wenyewe ZACCA.