Na Salum Vuai

Ni ukweli usiopingika kuwa, endapo kusingekuwa na michezo ambayo kimsingi huwaleta pamoja watu wa nchi, jamii, rangi na itikadi mbalimbali za kisiasa na kiimani, dunia isingekuwa pahala pazuri hata kidogo.

Bila shaka, dunia hii ingekuwa imejiinamia kwa huzuni, doro, isiyo na matumaini na iliyojaa kiza totoro.

Mbali na kujenga afya za wachezaji wa michezo mbalimbali, kutoa ajira kwao na burudani kwa watazamaji, michezo pia hutumika kuleta amani, upendo na kuheshimiana.

Michezo, iwe inayotangazwa/kuoneshwa moja kwa moja, ya mashindano, ya burudani au ligi, huwaruhusu watu kuepuka na kusahau kwa muda majukumu na shughuli zao za kila siku kwa dakika chache, saa mbili au wiki chache kutegemea na urefu wa muda wa michuano husika.

Huruhusu mivutano ya kisiasa, tofauti za kitamaduni na mikinzano yote kuwekwa pembeni, ili kutoa nafasi ya kuwaunganisha watu kimichezo kama vile Kombe la Dunia la mpira wa miguu linaloandaliwa na FIFA, michezo ya Olimpiki, mashindano ya mpira wa kikapu kimataifa chini ya usimamizi wa shirikisho la FIBA na mashindano mengine kadhaa.

Kunakuwa na hisia za umoja na upendo hasa wakati wa sherehe za ufunguzi wa mashindano makubwa kama ya FIFA, na katika kila mechi pale timu mbili zinapoingia uwanjani huku watoto wadogo wakishikana mikono kabla ya kupigwa nyimbo za mataifa ya timu zinazoshindana.

Kwa vile hakuna vurugu, vitendo vya kihuni na kukashifiana kati ya mashabiki wa timu pinzani, ni dhahri michezo hiyo huimarisha umoja na amani baina ya nchi na mabara.

Kwa mnasaba huu, michezo ina uwezo wa kuleta umoja na amani kwa dunia ambayo imegawika na kufarakana kutokana na tofauti za kidini na itikadi za kisiasa.

Hapana shaka, kupitia dunia ya michezo, tunaweza kuungana na kuwa wamoja bila kujali tofauti zetu.

Kwa kutambua umuhimu wa maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar ambayo yamewezesha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, katika siku za karibuni, Shirika la kimataifa la Internews limekuwa likishirikiana na jumuiya za waandishi wa habari visiwani Zanzibar, kuendesha kampeni maalum inayolenga kuelimisha umma juu ya haja ya kuandaa mijadala ya kuunga mkono juhudi za viongozi wakuu katika kuwaleta pamoja Wazanzibari, kuafiki maridhiano ili waijenge nchi yao.

Kupitia mikutano ya wadau, mafunzo kwa waandishi na kutumia vipindi vya redio na televisheni kuendesha mijadala yenye tija kwa ustawi wa Zanzibar na Wazanzibari.

Nami nimeona vyema nitumie nafasi hii kuviomba vyama vya michezo vilivyopo nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, kuangalia uwezekano wa kuandaa mashindano au mabonanza ya michezo kwa lengo la kuzidi kuwaunganisha wananchi baada ya maridhiano yaliyofikiwa hivi karibuni.

Historia inaonesha kuwa, michezo imekuwa ikitumika kuleta mafahamiano katika nchi na jamii mbalimbali ambazo ziliingia kwenye uhasama na ugomvi kwa sababu tofauti.

Mathalan, wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilipovunjika mnamo mwaka 1977, na kupelekea mpaka kati ya Kenya na Tanzania kufungwa, wanamichezo wa nchi mbili hizo waliendelea kutembelena na kushindana katika mashindano mbalimbali ikiwemo Kombe la Challenge.

Ni wazi kuwa katika ngazi ya kimataifa, siku hizi diplomasia haina nguvu kubwa katika kutatua migogoro na pale wanasiasa wanapogonga mwamba, wanamichezo wameendelea kuibuka kidedea katika kuleta suluhu na kuipatia ufumbuzi mizozo inayoonekana kuwa ni shida kuimaliza.

Marekani na China zilikuwa na uhasama wa kisiasa kwa miaka mingi uliopelekea viongozi wa mataifa hayo kutokuwa na mawazo ya kukutana ili kumaliza ugomvi wao.

Lakini hatimaye palichomoza kile kilichojulikana kama Diplomasia ya Pingpong (Mchezo wa mpira wa meza).

Chanzo chake kilikuwa katika mashindano ya kutafuta ubingwa wa dunia wa mchezo huo kwenye mashindano yaliyofanyika nchini Japan mwaka 1971, wakati Glenn Cowan wa Marekani na Zhuang Zedong wa China walipopambana na hatimaye wakawa marafiki wakubwa waliobadilishana zawadi nyingi na kuwasiliana mara kwa mara.

Urafiki wao ulipelekea viongozi wa nchi hizo kujiuliza; “Kama raia wa nchi zao wanaweza kuwa marafiki kwa nini wao wasijaribu kuelekea huko”.

Mifano ipo mingi lakini nitumie nafasi hii kuzishauri mamlaka za michezo nchini kuandaa mashindano au mabonanza ya michezo hata ya timu za maskani na barza za vyama mbalimbali kwa lengo la kujenga umoja na kumaliza tofauti za kisiasa miongoni mwao.

Ni matumaini yangu kuwa michezo hiyo ikiandaliwa vyema, itasaidia kupanda mbegu njema ambayo itakuja kuzaa matunda mema kwa manufaa ya Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.

Mashindano hayo yanaweza kujumuisha michezo kadhaa inayopendwa na wengi kama vile soka, netiboli, mpira wa kikapu na pia michezo ya jadi ikiwemo karata, bao, dhumna, kuvuta kamba, kufukuza kuku na kadhalika.

Wakati tukiendelea kushamirisha maelewano yetu, pia tuangalie raha itakayopatikana iwapo michezo itapewa nafasi yake katika kuongeza zege na kufanya maridhiano yetu yawe imara zaidi sasa na baadae.

Simu: 0777 865050/0714 425556

salumss@yahoo.co.uk