TU N A F A H A M U kuwa kila mwanadamu ana haki ya msingi ya kupata hifadhi, kuheshimiwa na hata kupewa ulinzi kuhusiana na maisha yake.

Lakini inapotokea hali anayokabiliwa nayo mtu ambaye si wa kawaida na inawezekana akahitaji msaada basi huyo ndiye anayepaswa kuangaliwa kwanza.

Tunapoangalia hali kama hizi tofauti suluhisho lake limewekwa kabisa kwa lengo la kuondosha unyonge kwa mtu anayehusika.

Kwa mfano, familia yenye watoto wengi inafaa yule mdogo kabisa ndio wa kupewa mapenzi ya juu kabisa.

Inapotokea kati ya watoto hao mmoja ni mgonjwa, basi huyo ndiye anayefaa kuoneshwa mapenzi makubwa zaidi. Huo ndio muafaka wa kugawa mapenzi kwa familia yenye zaidi ya watoto wawili.

Vyenginevyo mzazi anapaswa kuwapenda katika mizani sawa, ingawaje si wengi wanaoamini kuwepo kwa uzani huo. Katika hali ya kawaida masuala haya tunaishi nayo katika sehemu mbali mbali.

Haya tunayosema tunaishi nayo kwa sababu miongoni mwa watoto tunaoishi nao wanahitaji si mapenzi tu kwao, lakini pia wanahitaji uangalizi wa hali ya juu kwani wapo baadhi hali zaidi ama ni kutokana na maarifa ya kutofahamu namna ya kujishughulikia kwa watoto wenye ulemavu.

Kwa bahati mbaya sana, udhalilishaji watoto wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya udhalilishaji. Ingawaje hakuna takwimu zinazowajumuisha kundi hilo kuonesha ukubwa wa tatizo la udhalilishaji juu ya watoto hao wenye ulemavu ni jambo.

Katika hali isiyo ya kawaida na pengine isiyotegemewa, walemavu hasa watoto na wanawake wamekuwa waathirika wakubwa wa matendo ya udhalilishaji.

Kumekuwa na visa kadhaa vya walemavu wakinyanyaswa na kudhalilishwa kimapenzi kutoka na udhaifu wao wa kimaumbile, huku matukio mengine yakifanywa siri kwa kufiacha aibu.

Baadhi ya familia huwa zinajilazimisha kuyafanya siri na kuyaficha matukio hayo ya udhalilishaji kwa sababu wafanyaji ni miongoni mwa wanafamilia, hivyo muathirika kushindwa kupata haki zake.

Miongoni mwetu tumeshuhudia baadhi ya watu wanathubutu kuwapachika ujauzito watoto wenye ugonjwa wa akili, watoto hao wanakuwa hawajitambui na kubaki kulea ujauzito il-hali na wao wanahitaji kulelewa.

Hali kama hii inaondosha upendo kwa watu wenye ulemavu na inawezekana pia kutokana na maumbile yao ile dhana ya wazazi kuwaficha ikaongezeka maradufu.

Ifahamike kuwa wabakaji wana mbinu nyingi katika kutekeleza uhalifu wao, lakini kubwa zaidi endapo masuala haya hayachunguzwi na kusema na kila mmoja akawa na tahadhari juu ya mtoto wake.

Aidha baadhi ya watu wanawatoa kizazi watu wasiokuwa na akili kwa kuhofia kubakwa na kubebeshwa ujauzito hatua ambayo wakati fulani ilijadiliwa sana kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tuelewe kuwa kundi la watu wenye ulemavu wawe wanawake au wanaume wanapambana na changamoto nyingi.

Ni vyema masuala ya udhalilishaji yaanishwe kwa kundi hilo kwa lengo la kutafuta mwarubaini wa tatizo hili na kuepusha kuendelea zaidi kuwakumbwa watoto wa jamii hiyo.