NA JAALA MAKAME HAJI, ZEC

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imewaomba wananchi, wapiga kura wa jimbo la Pandani, vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kujitayarisha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliopangwa kufanyika Machi 28 mwaka huu.

Akizungumza na wadau wa uchaguzi katika ukumbi wa Jamhuri Wete Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alisema, uchaguzi huo unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mwakilishi mteule Abuubakari Khamis Bakary.

Mahmoud alieleza kuwa   uchaguzi huo hautakuwa na upigaji kura wa mapema kutokana na maelekezo ya sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mabruk Jabu Makame aliwaomba wapiga kura wa jimbo la Pandani kuendelea kudumisha amani mpaka kumalizika kwa uchaguzi huo.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo kaimu mkuu wa kitengo cha huduma za sheria Tume ya Uchaguzi, Mbaraka Said Hassouni alifahamisha kuwa, ZEC baada ya kupata taarifa kutoka kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi juu ya kuwepo nafasi wazi ya mjumbe wa Baraza la Wawakilishi inawajibika kuendesha uchaguzi huo kutokana na maelekezo ya kifungu cha 40(2) na (3) cha Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.

Nao wadau wa uchaguzi wa jimbo, wameishukuru Tume ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha vyema katika uchaguzi uliopita na kuiomba Tume hiyo kuendelea kuwashirikisha katika chaguzi zinazofuata.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetangaza kuwa Machi 12 mwaka huu kuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi Mdogo wa jimbo la Pandani na wadi ya Kinuni ambapo kampeni za uchaguzi zitafanyika Machi 13 hadi 26 2021.