By  Ali  Shaaban  Juma

UCHUMI wa buluu ni shughuli zote za kiuchumi zinazotokana au kuhusiana na bahari na fukwe za bahari. Tunapozungumzia bahari, tunakusudia bahari kuu zenye kina kirefu cha maji na bahari za kawaida zenye kina cha maji ya wastani.

Uchumi wa Buluu ni uhusiano uliopo kati ya bahari na  fursa  mbalimbali za kiuchumi zinazotokana  na  bahari.  Kwa lugha au tafsiri ya kiuchumi, uchumi wa buluu maana yake ni fursa zote za matumizi ya rasilimali za bahari kiuchumi kwa lengo la kuongeza pato la wananchi na taifa.

Uchumi wa buluu pia huangalia ulinzi wa mazingira na kuzingatia matumizi endelevu na sahihi ya rasilimali za bahari kiuchumi na kuhifadhi mazingira ili uchumi huo uwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha leo na kijacho.

Hivyo basi, Uchumi wa buluu endelevu ni uvunaji, uendelezaji na matumizi ya rasilimali za bahari wenye kutoa tija za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Uchumi wa buluu endelevu hujikita zaidi katika kuhakikisha kuwa uvunaji, uendelezaji na matumizi ya rasilimali za baharini unazingatia uhifadhi wa mazingira na viumbehai vya baharini kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye kulinda na kuhifadhi mazingira.

Asilimia 72 ya dunia tunayoishi imefunikwa na bahari ambayo inatoa ajira, chakula na maisha kwa zaidi ya asilimia 80 ya watu wote duniani.

Fukwe za bahari ambazo ni sehemu ya uchumi wa buluu zina mchango mkubwa katika kuchangia pato la sehemu kubwa ya uchumi wa dunia kwa vile fukwe hizo, mbali ya kupokea mamilioni ya watalii wanaotembelea sehemu mbalimbali duniani kila  mwaka, lakini pia hutoa ajira kwa mamilioni ya watu wanaohudumia sekta ya utalii. 

Utalii wa kimaumbile ambao kwa kiingereza unajulikana kwa jina la “sun, sand and sea”, kumaanisha “kuota jua, mchanga na kuogolea baharini” mbali ya kutoa ajira kwa watembezaji watalii, lakini pia ni fursa kwa wakaazi wa vijiji vilivyo kando ya bahari ya kufaidika kiuchumi kwa kutoa huduma kadhaa kwa watalii wanaofika maeneo hayo.

Pamoja na mambo mengine, uchumi wa buluu unajumuisha fursa za kiuchumi wa bahari ikiwemo uvuvi, ufugaji samaki, kamba, kaa, majongoo bahari, makombe ya baharini, chaza, pweza, ngisi na kilimo cha mwani.

Pia uchumi wa buluu unahusisha viwanda vya kushindika samaki, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali bandarini, miradi mikubwa ya maji pamoja na ujenzi wa vyelezo vya kujenga na kufanyia matengenezo meli na vyombo vyenginevyo vya usafiri.

Pia uchumi wa buluu unajumuisha utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi baharini na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia ya bahari.

Si hayo tu, bali pia uchumi huo wa buluu unahusisha kuyageuza maji ya bahari kuwa maji baridi yatakayotumika katika matumizi ya nyumbani na kumwagilia mashambani.

Miradi mingine mikubwa inayoweza kuanzishwa katika uchumi wa buluu na kutoa ajira kwa maelfu ya watu na kuongeza pato la taifa ni pamoja na kuanzisha miradi mkubwa ya uhifadhi wa mazingira na ujenzi wa miundo mbinu ya kuzalisha umeme utokanao na mawimbi ya bahari na upepo kando ya bahari.

Kwa mtazamo yakinifu, Uchumi wa buluu mbali ya kuangalia uvunaji wa rasilimali za baharini kwa lengo la kujiongezea mapato kutokana na rasilimali hizo, lakini kiutendaji, uchumi wa buluu ni kujenga na kutayarisha sera, mipango, miundombinu na kujenga uhusiano wa kikanda na kimataifa (interlink) kwa kuingia mikataba yenye lengo la kuwezesha matumizi ya fursa za makubaliano ya kikanda na kimataifa katika kufanikisha fursa za kiuchumi. 

Baadhi ya fursa hizo ni pamoja na usafirishaji wa bidhaa kwa meli kupitia bahari kuu, uvuvi wa meli kubwa katika bahari kuu na uvuvi wa meli ndogo katika bahari ya ndani. 

Miradi hiyo inaweza kufanikiwa kwa kuanzisha ubia wa uvuvi katika bahari kuu kati ya Zanzibar na makampuni makubwa ya uvuvi wa bahari kuu ambapo pia kwa kutumia utaratibu huo, taifa letu linaweza kuingia mikataba ya kimataifa ya uchimbaji wa mafuta, gesi na madini katika bahari zetu.

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Uchumi wa buluu hivi sasa unachangia wastani wa Dola Trilioni 24 duniani ambapo kiasi cha Dola Trilioni 2.5 zinapatikana kila mwaka duniani kutoka na huduma na mauzo yatokanayo na utalii, ufugaji wa samaki na viumbe wengineo wa baharini, usafirishaji wa bidhaa na abiria kwa meli na uvuvi.

Utalii wa mwambao ni moja kati ya nyanja kuu za uchumi wa buluu yenye kukua kwa kasi duniani hivi sasa. Inakisiwa kuwa wastani wa Dola Bilioni 6 hukusanywa kila mwaka na mataifa hasa ya visiwa kutokana na utalii wa matumbawe. 

Pato la uchumi wa bahari la mataifa yaliyo katika ukanda wa magharibi mwa bahari kuu ya hindi, (Western Indian Ocean Region) ambayo ni pamoja na Visiwa vya Comoro, Kenya, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Seychelles, Somalia, Afrika Kusini na Tanzania ikiwemo Zanzibar linakisiwa kuwa Dola 334 Bilioni.

Visiwa vya Unguja na Pemba vina eneo kubwa la uvuvi lenye kilomita za mraba 4,450. Aina mbali mbali za samaki wanapatikana katika bahari hiyo wakiwemo wale wenye soko kubwa kimataifa na wale wenye soko kubwa la ndani.

Jodari ni miongoni mwa samaki wenye soko kubwa kimataifa ambapo bahari ya Zanzibar ina aina mbalimbali za Jodari wanaoweza kuvuliwa katika bahari kuu na kuuzwa wabichi au walioshindikwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya utafiti ya “The Pew Charitable Trusts” ya mwaka 2018, biashara ya Jodari inachangia wastani wa Dola Bilioni 42 katika uchumi wa dunia kila mwaka.

Mbali ya aina mbalimbali za samaki, lakini pia kuna aina mbalimbali za viumbe wa baharini wakiwemo pweza, kaa, ngisi, chaza, matumbawe  na mwani  vyote vikiwa ni sehemu ya rasilimali zenye kutoa fursa katika uchumi wa buluu.

Kwa mujibu wa mtandao wa ResearchAndMarkets.com soko la kaa duniani litafikia tani Milioni 3.7 hapo mwaka 2026, ambapo China ndiyo mzalishaji mkuu wa kaa duniani.

Katika mwaka 2019, Marekani iliagiza kutoka nje kaa wenye thamani ya Dola Bilioni 1.38.

Wastani wa tani 2000 za samaki huvuliwa kila mwaka visiwani Zanzibar katika bahari za ndani za visiwa hivyo ambapo asilimia 14 ya watu wote hutegemea sekta ya uvuvi kuendesha maisha yao.

Hata hivyo eneo la bahari kuu ya Tanzania lenye ukubwa wa maili 200 bado halijagushwa na kuna maelfu ya tani za samaki ambao wanaweza kuvuliwa na kunufaisha taifa.

Kiuchumi, Zanzibar ambayo inakusudia kukuza uchumi wa buluu, ina fursa nzuri ya kutumia eneo tengefu la kiuchumi la bahari kuu (Exclusive Economic Zone), kuanzisha na kuimarisha uvuvi wa meli kubwa za kisasa.

Uchumi wa buluu ni fursa adhimu  ya kiuchumi inayoweza kutumiwa na Zanzibar kuwekeza miradi kadhaa mikubwa na midogo ya kiuchumi kwa wazawa na wageni katika uvuvi, ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, miundombinu ya uvuvi pamoja na usafirishaji wa mazao ya baharini yaliyosarifiwa katika kiwango cha kimataifa.

Katika kufanikisha azma ya kujenga Zanzibar yenye uchumi imara wa buluu, kunahitajika uwekezaji mkubwa katika uvuvi hasa kwa vile uvuvi unaotumika Zanzibar hivi sasa kwa asilimia kubwa ni uvuvi wa kienyeji wenye tija ndogo ulioajiri asilimia kubwa ya wavuvi wa kawaida.

Ili kufikia kiwango cha kuwa na uchumi buluu mkubwa wenye hadhi ya kimataifa na tija kwa taifa, wawekezaji wakubwa wa kimataifa katika sekta ya uvuvi wana nafasi nzuri ya kuwekeza visiwani Zanzibar kwa kuanzisha miradi mikubwa ya uvuvi wa bahari kuu.

Uvuvi wa kisasa katika bahari kuu na katika bahari za ndani, utaiwezesha Zanzibar kupata fedha nyingi zaidi ya zile zinazopatikana kila mwaka katika kilimo. Pia hatua hiyo itaongeza ajira kwa asilimia kubwa ya watu wa vijijini ambao hawana ajira.

Ujenzi wa miundombinu ya uvuvi ni eneo jengine ambalo Zanzibar inaweza kunufaika kutokana na uchumi wa buluu.

Uvuvi wa ndani na bahari kuu pamoja na ufugaji wa samaki utafanikiwa zaidi kama kutakuwa na uwekezaji katika ujenzi wa mitambo ya kuzalisha barafu ambayo ni muhimu katika kuhifadhi samaki na mazao mengineyo ya baharini.

Ni ukweli usiofichika kuwa boti zote za uvuvi zinazotumika hivi sasa Zanzibar ni zile zilizotengenezwa kwa mbao na mafundi wa kienyeji waliopo visiwani.

Katika kufanikisha uchumi wa buluu, boti kubwa za kisasa  zenye uwezo wa kwenda bahari kuu zitahitajika  hasa kwa vile uvuvi wa bahari kuu huwalazimu wavuvi kubaki mbali baharini kwa zaidi ya siku moja.

Hivyo basi fursa nyengine ya kiuchumi ambayo ipo Zanzibar katika kufanikisha uchumi wa buluu ni kuanzisha viwanda vya ujenzi wa boti za kisasa na meli ndogo za uvuvi. Lengo hilo litafanikiwa iwapo kutajengwa chelezo cha kisasa cha ujenzi wa meli na boti hizo za uvuvi.

Kwa upande mwengine moja ya kikwazo kikuu kinachochangia mapato madogo ya samaki miongoni mwa wavuvi wa Zanzibar, ni matumizi ya zana duni za uvuvi na upungufu wa zana hizo. Fursa ya kujenga kiwanda cha nyavu na zana nyenginezo za uvuvi ni njia nyengine ya kuimarisha uchumi wa buluu.

Mbali ya zana hizo za uvuvi kuuzwa hapa nyumbani, lakini pia zana hizo zinatuzwa nje ya Zanzibar. Uchumi wa buluu unakwenda sambamba na uvuvi wa kisasa unaotumia boti zenye kuendeshwa kwa mashine.

Kwa vile kutakuwa na boti na vyombo vingi vya uvuvi vyenye kutumia mashine, eneo jengine ambalo ni fursa ya kiuchumi ni ujenzi wa karakana ya kufanyia matengenezo mashine za boti za uvuvi.

Dhamira kuu ya uchumi wa buluu ni kuongeza na kuimarisha uvuvi wa kisasa na kuongeza mazao yatokanayo na uvuvi huo ili kukuza uchumi wa taifa na kuongeza kipato cha watu hasa wa vijijini.

Kwa vile matarajio ni kuongeza kiango cha samaki na mazao mengineyo ya baharini yanayovuliwa, kutakuwa na ulazima wa kuwepo kwa kiwanda cha kushindika samaki na mazao mengineyo ya baharini.

Hivyo basi, fursa nyengineyo ya kiuchumi inayoweza kuwepo kutokana na uchumi wa buluu ni ujenzi wa kiwanda cha kushindika samaki ambapo mbali ya samaki  hao kutumika katika mahoteli, lakini pia samaki hao waloshindikwa watasafirishwa nje ya nchi.

Kijografia, mazingira ya fukwe za visiwa vya Unguja na Pemba yanaruhusu ujenzi wa mabwawa ya ufugaji wa aina mbalimbali za samaki. Mito ya maji inayoingia mikokoni, ghuba, mapwaji ya bahari, vipwa vya maji pamoja na maji baridi  yaliyotuwama katika baadhi ya maeneo hasa kisiwani Pemba ni maeneo mazuri yanayoruhusu uazishaji wa mashamba na mabwawa ya ufugaji wa samaki.

Mbali ya mazingira hayo, lakini pia kuwepo kwa asilimia kubwa ya mimea na viumbe wengineo wa baharini ambao ni chakula cha samaki wanaofugwa kunatoa fursa ya ufugaji wa samaki visiwani humo kuwa wa gharama nafuu.

Kutokana na ukosefu wa utaalamu, mitaji, kutokuwepo ushauri na benki zenye kutoa mikopo kwa ajili ya uanzishaji wa miradi mikubwa ya ufugaji wa samaki na mazao ya baharini na uhakika wa soko bado eneo hilo halijafanyiwa kazi.

Hata hivyo, kuna fursa kubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya kuanzisha ufugaji wa samaki ambapo katika kufanikisha hilo, kuna haja kwa Wizara mpya ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kujifunza namna ya kufuga samaki kutoka kwa nchi kama Misri ambayo imefanikiwa sana katika hilo.

Pia wizara hiyo ina wajibu mkubwa wa kushirikiana na Taasisi ya Sayansi za Baharini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vyengine vya Uvuvi na masharika ya kimataifa ili kuandaa sera, mipango, mikakati na rasilimali watu ili kuona kuwa Zanzibar kama taifa na watu wake wanafaidika kwa kuanzisha mashamba na mabwawa ya ufugaji wa samaki, chaza, majogoo ya baharini, mwani, kaa, kamba pamoja na uyumba ambao ni chakula adhimu huko Asia. 

Kuwepo na uhusiano mzuri kati ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na vyombo vya habari kutasaidia sana kuiwezesha jamii ya Wazanzibari kufahamu kwa undani dhana ya uchumi wa buluu na kusaidia katika kutekeleza mikakati ya kufanikisha uchumi huo.

Wakati serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipodhamiria kukuza sekta ya Utalii, ilianzisha Chuo cha Utalii, Maruhubi ambacho kimesaidia kwa kiasi kikubwa kusomesha vijana kadhaa wa Zanzibar na nje ya visiwa hivyo ambao wanafanyakazi mahotelini.

Kwa lengo la kuwa na vijana wengi wenye ujuzi wa kutosha katika uchumi wa buluu, ni wajibu wa wizara husika kuchukua hatua za haraka kwa kushirikiana na taasisi za elimu za ndani na nje kusomesha vijana wa Kizanzibari ambao watafanyakazi katika nyanja zote za uchumi wa buluu.

Kazi hizo ni pamoja na uvuvi wa meli, ufugaji wa samaki, ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki, ushindikaji wa samaki, uhandisi wa meli, ujenzi wa boti pamoja na usarifu wa samaki na mazao mengineyo ya baharini (processing and packaging) kwa mujibu wa kiwango cha kimataifa.

Kaa waliovunwa nchini Indonesia wakiwa tayari kusafirishwa nje ya taifa hilo.

Samaki  aina ya Jodari  wakiwa katika mnada wa samaki hao huko nchini Japan.

Samaki   aina  ya  Perege baada ya  kuvunwa   katika  shamba la samaki huko Misri.