Wengi huathirika kisaikolojia, kiakili

Rais Dk. Mwinyi aagiza kuundwa mahakama ya udhalilishaji

NA MOHAMMED SHARKSY

KATIKA siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa wimbi kubwa la udhalilishaji na ukatili wa kijinsia hasa ubakaji katika jamii zetu jambo ambalo limewafanya wadau mbalimbali kukutana na rais hivi karibuni.

Ni ukweli usiopingika kuwa hakuna siku hata moja kusioripotiwa kesi hata moja inayohusu udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika vyombo vya habari.

Wimbi hili la ubakaji kwa kiasi kikubwa linazinyima raha familia, wahanga wa matukio na hata Serikali kwa ujumla.

Wako ambao hufanyiwa ukatili wa kijinsia wanaofariki, wanaojeruhiwa n ahata wanaoharibika kisaikolojia kwa muda mrefu kutokana na matendo hayo.

Kwa mfano hapa Zanzibar matukio kama haya huwakuta sana wanawake na watoto wa jinsia zote mbili yaani wanaume na wanawake kwa kubakwa ama kulawitiwa.

Hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya watuhumiwa lakini bado matendo hayo yamekuwa yakiripotiwa kila uchao.

Katika Makala haya ya afya leo yataangazia namna ya tatizo la ubakaji linavyotokea katika jamii zetu hapa zanizbar sambamba na hatua zinazochukuliwa.

NINI UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJISIA

Ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote ambacho kinaweza kusababisha madhara ya mwili, kingono au kisaikolojia au mateso kwa wanajamii, ikiwa ni pamoja na kutishiwa maisha, kunyimwa uhuru iwe hadharani au kwa kificho

UKUBWA WA TATIZO

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), iliyosomwa Ibrahim Mzee, alisema mwaka 2020 kesi walizopokea zilikuwa ni 531 na mikoa inayoongoza ilikuwa ni Mjini kwa kesi 248, Kaskazini kesi 58, Kusini kesi 80, Kaskazini Pemba kesi 64, Kusini Pemba kesi 81 huku kesi walizopeleka mahakamani zilikuwa 404 mafaili 110 walitoa maamuzi yaendelee na upelelezi na mafaili 43 yalikuwa hayana ushahidi.

Aidha alisema kesi 414 zilifunguliwa mahakamani ikiwemo wilaya, Mkoa na mahakama ya watoto, kesi 62 zilitiwa hatiani, walioachiwa huru 43 zilizoondoshwa 51 na kesi zilizoondoshwa na upande wa mashitaka zilikuwa kesi saba.

Aidha alibainisha kuwa changamoto ya kisheria inasababisha kuongezeka kwa makosa ya udhalilishaji nchini.

ALICHOKISEMA RAIS DK. MWINYI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyi alisema tatizo la udhalilishaji ni kubwa na linaleta aibu katika nchi na maumivu makubwa kwa wananchi walio wengi na lisipokemewa litaendelea kuharibu watoto.

Alisema lipo tatizo la msingi linalohitaji ufumbuzi kwa kushirikiana pamoja ikiwemo serikali, wananchi, mahakama, Ofi si ya DPP, Jeshi la Polisi ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii ili kukinga tatizo hilo kabla halijatokea.

Aidha Dk. Shein alisema anatambua wapo wanaharakati, viongozi wa dini, masheha, waratibu na taasisi zisizo za kiserikali wanafanya kazi katika jamii, lakini tatizo linaendelea kuwepo hivyo imefika wakati kuchukuliwa hatua kali dhidi yao. Hata hivyo, alisema bado taasisi zote zina jukumu la kurekebisha kasoro zao ikiwemo polisi kuacha kupatanisha kesi hizo baina ya mkosaji na aliyekosewa kifamilia.

Dk. Mwinyi alizitaka taasisi zote ikiwemo mahakama, polisi na ofi si ya Mkurugenzi wa Mashitaka kujipanga upya ka ka kukabiliana na ta zo hilo ili lisiendelee kupoteza nguvu kazi ya taifa.

“Bado kazi ya ziada inahitajika katika mahakama kwa kuhakikisha wanapunguza muda wa kufuatilia kesi hali ambayo inapelekea wananchi kukata tamaa kufuatilia kesi zao”, alisema.

Hata hivyo, alisema wakati umefika kufumua sheria ambazo zinakuwa kikwazo katika masuala hayo kwa kuja na sheria muafaka ka ka kukomesha vitendo hivyo.

Dk. Mwinyi aliwaagiza wale wote wanaoshughulika na masuala ya sheria serikalini kukaa chini na kulifanya jambo hilo kwa haraka ili Baraza litakalokaa mwezi wa Februari mwaka huu liende na mabadiliko ya sheria hizo.

WANAHARAKATI WANASEMAJE

Amina Yussuf Ramadhan ni mwanaharakati wa kupinga masuala ya udhalilishaji alisema yapo makundi yanayosababisha kuunga mkono masuala hayo kwa kutaka suluhisho katika ngazi za kifamilia.

Akizungumzia vichocheo vinavyosababisha kuongezeka kwa matukio hayo alisema ni wingi wa baa katika makaazi ya watu, mmong’onyoko wa maadili, vituo vya polisi kuwa gesti bubu na utalii usiozingatia maadili ya kizanzibari.

Akizungumzia mafanikio waliyoyapata alisema ni pamoja na jamii kupata muamko juu ya kuripoti matukio hayo na kudai haki zao pale wanapokosa na kuweza kusaidia wahanga 200 kurekebisha tabia zao.

Nao washiriki wa mkutano huo walisema imefika wakati kuwa na uwazi katika kusimamia matukio hayo kwa kuweka mikakati maalum ili kuondoa vitendo hivyo.

Dk. Mzuri Issa kutoka chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar alisema sheria ina mapungufu mengi ikiwemo sheria ya ushahidi ambazo zimekuwa zikikinzana kwa kiasi kikubwa.

Naye Jamila Mahmoud kutoka chama cha wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) alisema rushwa inachukua nafasi kubwa ka ka kutoa haki ka ka vitendo vya udhalilishaji hivyo alishauri kushirikiana pamoja kila mmoja kwa nafasi yake ka ka kuliondoa ta zo hilo.

SABABU ZA UDHALILISHAJI (UBAKAJI)

Pamoja na mambo mengine lakini tendo la ubakaji ambalo dini zote hulipinga ni moja ya matendo ya laana na ujinga uliokithiri unaofanywa na baadhi ya wanaume.

Baadhi ya wabakaji ni wagonjwa wa akili, wanaume wengine wanabaka kwa sababu wanafikiri wanawake wako pale ili kuwaridhisha wao katika masuala ya kujamiiana, na kumwadhibu msichana, mwanamke n ahata watoto wadogo.

Utumiaji wa dawa za kulevya na pombe vinaweza kuwa ni vishawishi vikuu vya ubakaji kwani vinaweza kumshawishi mbakaji baada ya kushindwa kujizuiya kutokana na kuwa anachokifanya hakiko katika akili yake.

Aidha Ushawishi na Ulaghai kwa baadhi ya watoto na wasichana ni mambo yanayopelekea kukutwa na matendo hayo bila ya ridhaa ya mtu husika.

Mara nyingi wasichana wanaobakwa wakiwa chini ya umri wa miaka 18 hubebeshwa ujauzito na wakati mwengine kurukishwa virusi vya ukimwi bila ya kujua.

Hali hiyo kwa baadhi ya wasichana hupelekea kukata tamaa na kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata mimba na kuolewa katika umri mdogo.

Sambamba na hilo mara baada ya ubakaji kinachopelekea kwa baadhi ya wasichana huthubutu kuwaua ama kuwatupa watoto wakiwa wachanga na kupelekea kupoteza maisha.

ATHARI ZA UBAKAJI KIAFYA

Kuchanika sehemu za siri za mwanamke au hata wanaume wanaolawitiwa pamoja na kupata maumivu sehemu ya siri (Lacerations and internal injuries)

Mimba zisizotarajiwa (Unwanted pregnancy) matokeo yake kutoa mimba kusiko salama (unsafe abortion etc)

Kupata magonjwa ya Ngono, kama vile Gono, kaswende na maambukizi ya virusi vya ukimwi, matatizo ya viungo vya siri, matatizo ya kisaikolojia na kutengwa na jamii kwa baadhi ya wahanga.

Athari nyengine ni pamoja na kupatwa na msongo wa mawazo na hatimae kujiua (Fear, depression, and suicide)

Kuwa na tabia mbaya kama kulipiza kisasi, matumizi ya madawa ya kulevya, ubarazuli, kuendelea kufanya ngono zembe na hata kuamua kuambukiza wengine kwa makusudi ni mambo yanayotokana na athari za kubakwa.

Matatizo mengine ni kutotembea sawasawa, kutokwa na uchafu na kuoza sehemu za siri, kuwashwa sehemu za siri.

Kushindwa kuzuia choo kikubwa na kidogo kutokana na kuathirika sehemu za siri pamoja na michubuko na vidonda sehemu ya siri ni mambo yanayoiweza kumpata mtu aliebakwa.

MAMBO MUHIMU YA KUYAFANYA

Mara nyingi mtu aliebakwa anatakiwa kupatiwa huduma za dharura na zaharaka ipasavyo na ikiwezekana mara tu baada ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kupatiwa huduma ya dawa za PAP ambazo zinaweza kuepusha maambukizi ya ukimwi.

Pia kupatiwa ushauri nasaha sambamba na tiba sahihi kwa muhanga wa matukio ya ubakaji.

Aidha jamii inapaswa kuweka ushahidi hasa kwa watoto wanaobakwa ikiwa ni pamoja na kutowasafisha huku wakitakiwa kuwahi kuwapeleka polisi kwa ajili ya kupewa fomu ya polisi ya PF3 kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu.

Kuwakinga na mimba zisizo tarajiwa hasa kwa wasichana walikuwa wameshabaleghe.

Kupatiwa ushauri wa kisheria na kusaidiwa kesi kupelekwa Polisi ili hatimae kwenda makahakamani na Kupatiwa ufumbuzi wa tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kumtia hatiani mtendaji wa kosa hilo.

Jamii kutokubali mapatano ya aina yoyote kwa mtu alietekeleza udhalilishaji au ubakaji jambo ambalo linaweza kusababisha kuongezeka kwa matendo hayo.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa kukishuhudiwa watoto wengi wanaobakwa. Kulawitiwa au udhalilishaji wa aina yoyote kukatishwa masomo ama kunyanyapaliwa jambo ambalo humkosesha haki yake ya msingi.

NINI KIFANYIKE

Hivyo jamii inashauriwa kukutana na taasisi husika kama elimu, afya na wanaharakati na kueleza kwa kina tatizo ili mtoto kutopata matatizo sambamba na kumuhamisha mtoto kutoka katika skuli moja na kumpeleka nyengine.

Kuepuka ndoa za mapema kwa wanafamilia ikiwa ni pamoja na kutokubali mapatano ya kuolewa jambo ambalo linachangia kuendelea na udhalilishaji wa kijinsia na kuongezeka matendo hayo.

Wanaharakati kuendelea kutoa taaluma dhidi ya matendo hayo ili watuhumiwa waweze kutiwa hatiani.

Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali kuimarisha mitaala ya somo la stadi za maisha na athari zake ili wanafunzi wafahamu kwa kina athari za ubakaji, mimba za utotoni, ndoa za mapema na maambukizi ya virusi vya ukimwi na maradhi ya kujamiana.

Aidha wizara ya elimu kurekebisha sheria ya elimu kuhusiana na kifungu cha adhabu kwa wabakaji, ndoa za mapema ili kuleta tija kwa wahanga wa matukio hayo.

Viongozi na jamii wana wajibu mkubwa wa kuielimisha jamii kuhusu sababu aina na athari za ukatili wa kijinsia na ubakaji.

Elimu ya udhalilishaji na ubakaji itatoa mchango mkubwa katika kubadilisha mitazamo na matendo kwa wanajamii.

 Kwa ushirikiano tunaweza kubadilisha mitazamo ya wanajamii kuhusu usawa wa kijinsia na kutoa michango yao kupiga vita unyanyasaji na ubakaji.

Wazazi wana wajibu wa kufuatilia mienendo yawatoto wetu, kuongeza ulinzi kwa watoto na kuepusha ubakaji na udhalilishaji katika jamii zetu.

Hayo yote yatawezekana ikiwa kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atatekeleza wajibu wake ipasavyo.