KAMPALA,UGANDA

SERIKALI ya Uganda imefunga mitandao ya kijamii ikiwa imebakia masaa machache  kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi.

Serikali ya Uganda iliagiza watoaji huduma za mtandao kufunga mitandao yote ya kijamii na programu za kutuma ujumbe kufikia Jumanne kwa muda usiojulikana.

Hiyo ni kwa mujibu wa barua kutoka kwa mdhibiti wa mawasiliano nchini humo iliyonukuliwa.

Watumiaji walilalamika kwamba hawawezi kupata mtandao wa Facebook na WhatsApp, majukwaa ya mitandao ya kijamii inayotumiwa sana katika kipindi cha kampeni kabla ya uchaguzi wa urais kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

“Tume ya mawasiliano Uganda inaagiza kusitisha ufikiwaji na utumiaji, wa moja kwa moja au kinyume chake, kwa mitandao yote ya kijamii pamoja na programu za kutuma ujumbe mitandaoni kwa muda usiojulikana,” ilisema sehemu moja ya barua kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume  ya Mawasiliano ya Uganda kwenda kwa watoaji huduma za mtandao.

Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilitangaza kuwa, zaidi ya raia milioni 18 walitimiza masharti ya kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa kesho.