KAMPALA, UGANDA

UGANDA imeikosoa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo alisema Marekani inajaribu kudumisha na kudhalilisha mchakato wa uchaguzi wa urais wa wiki iliyopita.

Hiyo ni baada ya Balozi wa Marekani mjini Kampala, Natalie E Brown kujaribu kumtembelea kinara wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi huo,Robert Kyangulani maarufu kama Bobi Wine katika makaazi yake.

Hata hivyo mwanadiplomasia huyo wa Marekani nchini Uganda alizuiwa na maofisa usalama kuingia katika makaazi hayo ya Wine viungani mwa mji mkuu.

Msemaji wa serikali ya Uganda alisisitiza kuwa,alichojaribu kufanya Brown ni kuingilia wazi mambo ya ndani ya Uganda, na hususan uchaguzi wao.

Opondo alisema balozi huyo wa Marekani mjini Kampala hapaswi kufanya jambo lolote linalokwenda kinyume na taratibu na majukumu yake ya kidiplomasia.

Tume ya Uchaguzi Uganda ilimtangaza rasmi Yoweri Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi, kwa kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote wakati mpinzani wake wa karibu, Bobi Wine akipata kura milioni 3.48 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.