NA MWANAJUMA MMANGA
WANANCHI wamelalamikia hospitali ya Mnazi mmoja kuwepo kwa uhaba wa damu kwa mama wajawazito hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili wananchi hao wamesema tatizo hilo lipo na wanapoenda na wagonjwa wao wajawazito huwa wanaambiwa warudi wakachangie damu ili kusaidiwa mgonjwa wao.
Mmoja wa mama ambae mwanawe amelazwa Hospitali ya mnazi mmoja, Asha Ali Juma, alisema kinachoshangaza mgonjwa kishafika hatua ya kuzalishwa anaambiwa damu hana hivyo ameiyomba serikali kutafutwa mbinu nzuri ya utafutaji wa damu za akiba ili kuokoa mama wajawazito.
“Nasikitishwa na kitendo cha kuwambiwa kusubiri mama huku uchungu ushaanza unaambiwa itabidi azalishwe kwa upresheni huku damu aliokuwa nayo haitoshi kitu ambacho ni cha kubahatisha maisha” alisema mama huyo.
Nae Afisa Uhamasishaji Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Omar Said Omar, amekiri kuwepo kwa uhaba wa damu katika vituo vya afya ambavyo vinazalisha ikiwemo Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Alisema katika mazingira waliokuwa nayo walikuwa na tatizo la uhaba wa fedha kidogo lakini hivi sasa fedha tayari wameshaingiziwa na shughuli zimeanza.
Alisema benki hiyo imeamua kufanya zoezi la uchangiaji wa damu jana huko Kisonge ambapo ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kutimiza mika 57 ili kukabiliana na uhaba wa damu.
“Wananchi waache kutoa malalamiko pale wapokosa damu na badala yake kuhamasika kujitokeza kwa wingi pale inapofanyika zoezi la uchangiaji damu ili kupatikana damu ya akiba nay a kutosha” alisema afisa huyo.
Alisema katika zoezi hilo Benki ya damu Salama imefanikiwa kupata unit 170 ambazo wamezikusanya na wameweza kwenda nazo katika benki kwa ajili ya kuzichunguza na kuzihifadhi.
Alifahamisha kuwa mahitaji ya damu kwa mwezi ni chupa 1550 lakini hali hiyo ipo chini ya kiwango kutokana na ukusanyaji mdogo hivyo amewataka wananchi kuchangia damu kwa hiyari kwani kutasaidia kuokoa maisha ambao wanaopata ajali na akinamama wajawazito.
Alisema wanamikakati kwa wanajamii kuhamasisha kujitokeza kuchangia damu na kuwa tayari kutoa mashirikiano na benki hiyo, ili kupata damu ya hakiba.