TIGRAY, ETHIOPIA
MJUMBE maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji wa kingono Pramila Patten amesema tuhuma nzito zimeibuka, kwamba uhalifu wa kingono ulifanyika katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Alisema katika ripoti yake kuwa wanawake na wasichana kwenye jimbo hilo walipungukiwa na vifaa vya kuhifadhi ushahidi wa kubakwa na pia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi.
Katika taarifa yake Patten amenukuu taarifa kwamba baadhi ya wanaume walilazimishwa kuwabaka wanawake kutoka ndani ya familia zao, la sivyo wakabiliwe vitisho kwa maisha yao.
Hali kadhalika, ripoti hiyo iliyochapishwa hapo juzi ilidai kuwa badhi ya wanawake walilazimishwa kufanya ngono na wanajeshi kabla ya kupatiwa mahitaji ya lazima.
Tarifa hiyo iliongeza kuwa takwimu kutoka hospitali za jimbo hilo zinaonyesha ongezeko la watu wanaotaka vidonge vya kuzuia mimba, na wanaotaka kupima magonjwa yanayoambukizwa kupitia matendo ya ngono.