NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Uhamiaji imefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi daraja la kwanza Kanda ya Unguja baada ya kufikisha pointi 13.

Timu hiyo imefikia hatua hiyo baada ya juzi kuifunga Idumu mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa uwanja wa Bungi.

Mbali na mchezo huo pia katika uwanja wa Amaan Kilimani City na Mchangani United zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilicheza kwa kushambuliana mara kwa mara na kukamiana kwa kila mmoja kutaka kuondoka na ushindi.

Kwa matokeo hayo Kilimani City imefikisha pointi 10 nafasi ya nne na Mchangani inaendelea kudima katika nafasi yake ya mwisho ikiwa na pointi tano.

Mabao ya Kilimali City yalifungwa na Ahmed Seif (Chapweza) dakika 19 na Abdilah Seif Bausi dakika ya 46 kwa penalti na Mchangani mabao yake yalifungwa na Salum Ahmed dakika 29 kwa penalt iliyosababishwa na Ali Seif Bausi kuunawa mpira na la pili lilifungwa na Salum Ahmed dakika 54.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo nafasi ya pili inashikiliwa na Ngome wenye pointi 10 akifuatiwa na Taifa ya Jang’ombe yenye pointi 10 pia lakini timu hizo zipo nyuma kwa mchezo mmoja.