LONDON, UINGEREZA

UINGEREZA inatarajiwa kutangaza kuwa itajiunga na mataifa mengine duniani ikiwemo Misri, Bangladesh, Malawi na Uholanzi kuzisaidia jamii ulimwenguni zinazokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.

Serikali ya Uingereza iliarifu kuwa msimamo huo utatangazwa na waziri mkuu Boris Johnson wakati atakapohutubia mkutano wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi chini ya wenyeji wa Uholanzi.

Kulingana na ofisi ya Waziri mkuu, Johnson atazungumzia umuhimu wa nchi hiyo kushirikiana na madola mengine kuzipiga jeki jamii zilizo kwenye hatari kupambana na ukame, majanga ya asili pamoja na ukosefu wa chakula.

Muungano huo wa mataifa utalenga kuwatumia wanasayansi, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia kupata ujuzi na njia mwafaka za kikanda na kilimwengu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.