BERLIN,UJERUMANI

GAZETI la Ujerumani la Bild limeripoti kuwa polisi imeimarisha usalama katika majengo ya bunge ya Ujerumani mjini Berlin kufuatia uvamizi uliotokea katika majengo ya bunge nchini Marekani.

Gazeti hilo limenukuu barua ya Rais wa Bunge la Ujerumani Wolfgang Schaeuble kwa wabunge nchini humo.

Schaeuble alitaka ripoti kutoka ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani juu ya ghasia zilizotokea katika majengo ya bunge nchini Marekani na kuwa serikali itatoa mwelekeo zaidi na mafunzo watakayoyapata katika uvamizi wa Marekani ili kulilinda bunge.

Msemaji wa polisi alisema watachukua hatua zaidi ili kuimarisha usalama katika majengo muhimu mjini Berlin, akiashiria jengo la Reichstag lenye makao ya bunge ya Ujerumani na sehemu zenye mafungamano na Marekani.