Yaahidi kulirejeshea hadhi yake

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ameukaribisha utayari wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kushirikiana na serikali katika ujenzi wa jengo la Beit al Ajaib.

Dk. Mwinyi aliyasema jana ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya  mazungumzo na Mwakilishi wa shirika hilo nchini Tanzania, Tirso Dos Santos.

Alimueleza Mwakilishi huyo wa UNESCO kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini ushirikiano uliopo na Shirika hilo, hivyo hatua hiyo ya kuiunga mkono Zanzibar katika  kulifanyia matengenezo jengo la Beit al Ajaib ni uthibitisho mkubwa.

Alisema serikali imeanza kuchukua hatua baada ya jengo hilo kuporomoka ikiwa pamoja na kuunda kamati ya uchunguzi ambayo itabainisha kile kilichosababisha kuporomoka kwa jengo hilo la kihistoria.

Dk. Mwinyi alitoa ushauri kwa UNESCO wa kuyafanyia tathmini majengo yote ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ili yasiendelee kuleta athari zaidi.

Alisema kuwa azma na utayari wa UNESCO kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kulijenga jengo hilo la kihistoria ina umuhimu mkubwa katika kuurejeshea hadhi yake Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni urithi wa dunia.

Dk. Mwinyi alifurahishwa na azma ya shirika hilo la kuwaleta wataalamu kwa awamu tatu hapa Zanzibar ambapo kila awamu itakuwa na wataalamu wake ambapo inaonesha azma sahihi ya UNESCO ya kushirikiana na Zanzibar.

Alimueleza Mwakilishi huyo kwamba serikali itahakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa timu za wataalamu watakaokuja kufanya shughuli hiyo hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya shughuli zao.

Kwa upande mwengine, Dk. Mwinyi  alilipongeza shirika hilo kwa azma yake ya kulifanyia ukarabati jengo la sinema ya Majestic ambapo tayari nusu ya fedha za ukarabati huo zimeshapatikana.

Alieleza kuwa shirika hilo limeweza kushirikiana na Zanzibar kwa muda mrefu hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa miradi mbali mbali ambayo (UNESCO) inaiunga mkono ikiwemo miradi ya elimu, utamaduni, afya na mengineyo ambayo imepata mafanikio makubwa hapa Zanzibar.

Awali Mwakilishi huyo wa UNESCO, Tirso Dos Santos, alimueleza Dk. Mwinyi kuwa shirika hilo lina azma ya kulifanyia matengenezo jengo la Beit-al -Ajaib ili lirudi katika uhalisia wake kwa kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwakilishi huyo, alimueleza Dk. Mwinyi kuwa shirika hilo litaanza kuleta wataalamu wake kwa ajili ya mradi huo ambao wataanza kuja mnamo Januari 18 mwaka huu ambao watakuja kwa awamu tatu ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafanikiwa tena kwa muda uliopangwa na ufanisi mkubwa.

Alimueleza Dk. Mwinyi kwamba UNESCO itahakikisha inafuata taratibu zote katika kuhakikisha ujenzi huo unafanywa kwa taratibu zote za Kimataifa bila ya kuathiri mambo mengine.

Mwakilishi huyo wa UNESCO, alimueleza Dk. Mwinyi kwamba baada ya timu hizo za wataalamu kukamilisha kazi zao ujenzi wa jengo hilo utaanza mara moja huku akimueleza kuwa amepokea ushauri na wazo la kuyafanyia tathmini majengo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Mwakilishi huyo alimpa salamu za rambi rambi zilizotumwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Audrey Azoulay na Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Urithi wa Dunia Bi Mechtild Rossier kufuatia kuporomoka kwa jengo la Beit al Ajaib na kupelekea vifo pamoja na majeruhi kadhaa.

Alitoa pongezi kwa Dk. Mwinyi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 huku akisisitiza UNESCO, itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbali mbali ili iweze kuleta tija na ufanisi.

Sehemu kubwa ya jengo la  Beit el Ajaib liliopo Forodhani Jijini Zanzibar ambalo ni miongoni mwa majengo ya urithi wa dunia ambapo pia, ni miongoni mwa majengo yanayotambuliwa na UNESCO liliporomoka mnamo Disemba 25, mwaka jana 2020.