NA ZAINAB ATUPAE
UONGOZI wa jimbo la Malindi, umesema utakuwa bega kwa bega na walimu wa skuli ya Hurumzi, kuondoa vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo.
Wakizungumza na wananchi pamoja na walimu wa skuli hiyo huko shehiya ya Hurumzi katika muendelezo wa kusikiliza changamoto za wanchi wa jimbo lao.
Walisema ipo haja kubwa ya kuliingilia kati suala hilo,ili kuwasaidia vijana wao kupata elimu itakayo wasaidia katika maisha yao ya baadae.
Walisema wanafunzi wanashindwa kukaa darasani kuwasikiliza walimu wao na kutumia muda mkubwa kukaa nje na kujiingiza katika matendo yasiokuwa na msingi, ikiwemo kuvuta sigara, kuangalia picha za ngono pamoja na kuaa baharini kupiga makachu.
Walisema vitendo hivyo vinasababisha wanafuzi kufanya vibaya na kuipa sifa mbaya skuli hiyo kwa kutoa matokeo mabaya.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake wa skuli hiyo Fatma Ali, alisema wamechoshwa na matendo hayo na kuwataka viongozi kulingilia kati, ili kuwasaidia vijana wao.
“Unakuja darasani unakutana wanafunzi 20 na hoa siku nyengine wanakuwa wengi wakati njiani umepishana nao wanazurura tu, hili kwakweli tumechoka walimu,”alisema.
Asha Haji Mohamed, ni miongoni mwa wazazi mwa wanafunzi ambao wanasoma skuli hiyo, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, hivyo aliwataka wazazi wenzake kuwaunga mkono, ilikuwasaidia vijana wao.
Mohamed Suleman Omar, ni Mbunge na Mohamed Ahamada, ni mwakilishi wa jimbo hilo, walisema kwa upande wao watungana kuondoa changamoto hiyo na kuwataka wanafunzi kusoma kwa bidi, ili baadae kuwa wafanyakazi wazuri wa nchi yao.