MOSCOW,URUSI

IDARA ya magereza nchini Urusi imesema italazimika kumkamata mara moja kiongozi wa upinzani Alexei Navalny iwapo atarejea nchini humo Jumapili kama alivyopanga.

Idara hiyo ilidai kuwa mkosoaji huyo mkubwa wa Rais Vladmir Putin alikiuka masharti ya kifungo chake.

Navalny kwa sasa yuko Ujerumani tangu alipopewa sumu inayoharibu mishipa ya fahamu mwezi Agosti mwaka 2020.

Navalny, mwenye umri wa miaka 44 aliugua akiwa ndani ya ndege akitokea Siberia kwenda Moscow na baadae alipelekwa Berlin kwa matibabu.

Kiongozi huyo wa upinzani anadai kuwekewa sumu na Putin, madai ambayo yalikanushwa na Ikulu ya Urusi.

Idara hiyo ya magereza ilisema tayari imeiomba mahakama ya Moscow ibadilishe hukumu yake kuwa kifungo gerezani.

Aidha, inadai Navalny alikiuka masharti mara sita kwa kushindwa kujisajili kwa maofisa mwaka uliopita, kama sehemu ya hukumu ya kifungo cha nje iliyotolewa mwaka 2014.