NA MWANDISHI WETU

MNAMO Disemba 31 wiki iliyopita, Zanzibar iliadhimisha siku ya usafi kitaifa ambapo maeneo mbalimbali ya wazi yalisafishwa na kuwa katika mazingira ya kupendeza.

Zoezi hilo la usafi liliongoizwa na vikosi vya SMZ, watumishi wa serikali za mitaa, vikundi vya usafi pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ikiwa ni moja ya shamrashamra ya kuelekea sherehe za Mapinduzi Zanzibar.

Hata hivyo, licha ya usafi kuwa jambo muhimu lililohimizwa na vitabu vya dini ili mja alitekeleze bado, limekuwa ni suala zito hasa katika maeneo ya makaazi.

Tabia hiyo imekuwa ikirudisha nyuma juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vilivyokabidhiwa dhamana ya kusimamia ikiwemo Baraza la Manispaa ya mjini.

Bila ya shaka uzito huo, unakuja pale baadhi ya watu kutokuwa tayari kufuata maelekezo yanayotolewa na chombo hicho ikiwa ni pamoja na utupaji wa taka ovyo uliokithiri baadhi ya maeneo.

Wapo wanaodhani chombo hicho ndicho chenye jukumu pekee la kuweka mazingira safi na kusahau ya kwamba dini inasema usafi ni wajibu wa kila mmoja.

Pamoja na mambo mengine lakini Baraza la Manispaa hasa Mjini limeandaa mikakati kadhaa iliyo bora ikiwa ni pamoja na uwekaji wa ndoo maalumu kutupia taka na matangazo maeneo mbali mbali ambayo bila ya shaka yatasaidia kutoa wito kwa jamii.

Ipo haja ya jamii kuendeleza usafi na kuwa ni tabia na kwamba isisubiri tu siku la zoezi la kitaifa la kuweka mazingira safi ndio wafanye usafi.

Ikumbukwe utalii Zanzibar unachangia asilimia 27 ya pato la taifa hivyo ipo haja ya kuweka mji wetu safi kwani ndio roho na kiini cha uchumi wa taifa.

Kwa upande mwengine ni jambo la aibu nchi kama Zanzibar, kusikia imefeli kiusafi hasa ikizingatiwa ni miongoni mwa visiwa vyenye historia nzuri katika mataifa mengine duniani.

Isitoshe wapo baadhi ya wananchi hapa nchini husikika wakisifia mji wa Arusha kwa usafi sambamba na kuponda visiwani mwao bila ya kutafakari au kujiuliza kwanini wao waliweza na vipi sisi tushindwe?

Nafikiri si wakati wa kuonesheana vidole jambo la msingi tushikamane sote kwa pamoja kuweka mji wetu safi kwani “kidole kimoja hakivunji chawa”.

Bila ya shaka penye nia pana njia hivyo ni wakati wa kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na baraza hilo, hakika ni njema na zina manufaa kwa taifa letu ambalo linahitaji maendeleo ya haraka.

Ifahamike bila ya wananchi wenye kujenga tabia ya kuimarisha usafi ni vigumu kufikia malengo kwani sio rahisi mgeni kubadilisha mazingira yaliopo.

Ni ukweli usiopingika, usafi ndio ustawi wa maendeleo popote duniani hivyo, Wazanzibari ni vyema kushajihishana, kukumbushana kwani uchafu ni chanzo cha maradhi mbali mbali ikiwemo yale hatari ya kipindupindu.