KIZAZI cha vijana wenye miaka 30 kushuka chini, hakimjui mtawala mwingine katika taifa la Uganda zaidi ya Yoweri Kaguta Museveni ambaye yupo madarakani kwa takriban miaka 35.

Museveni anaingia katika orodha ya viongozi waliohudumu madarakani kwa muda mrefu barani Afrika, akiungana na mzee Paul Biya ambaye ni rais wa Cameroon, ambaye yupo madarakani tangu mwezi Novemba mwaka 1982.

Orodha hiyo pia inamjumuisha Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, Rais wa Equatorial Guinea, ambaye amekalia kiti cha urais tangu mwezi Agosti mwaka 1979.

Ushindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini Uganda, unamuweka Museveni kwenye orodha hiyo huku akitarajiwa kuuanza muhula wa sita baada ya kutangazwa mshindi.

Akitangaza matokeo, mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi ya nchini Uganda, Simon Mugenyi Byabakama, alisema Museveni ameshinda uchaguzi uliofanyika Januari 14 mwaka huu, kwa kupata asilimia 58.6 ya kura zote.

Museveni kwa karibu sana alifuatiwa na mwanasiasa kijana ambaye ametokea kwenye tasnia ya muziki kabla ya kuingia kwneye siasa, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine aliyepata asilimia 34.8.

Katika eneo la Afrika Mashariki, umekuwepo uraibu kwa baadhi ya viongozi kukaa madarakani muda mrefu, ambapo hufanyika mabadiliko ya katiba ili waendelee kuwepo na mara nyingi mabadiliko hayo huleta fujo au manung’uniko.

Kwa mfano marehemu Pierre Nkurunziza aliyekuwa rais wa Burundi, alifanya hivyo rais wa Rwanda Paul Kagame amefanya hivyo n ahata Yoweri Museveni wa Uganda naye amefanya hivyo.

Kwa hakika Kagame na Museveni hakuna ajuaye lini wataviachia viti vya urais, kwa sababu mabadiliko ya kikatiba waliyoyafanya kwenye katiba za nchi zao hayana ukomo wa kuondoka madarakani.

Katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni nchini Uganda kumeshuhudiwa mambo mengi ambayo mengine yanatia shaka kusema hadharani kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Pamoja na kwamba kundi la waangalizi wa uchaguzi huo kutoka nchi za Afrika Mashariki kueleza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki, hata hivyo wameshindwa kukosoa hata kadhia ya kuzimwa kwa huduma ya intaneti.

Bob Wine, mgombea mkuu wa upinzani alisema uchaguzi haukuwa huru na haki na kwamba anao ushahidi wa madai yake na anasuburi muda muafaka ili awaoneshe waganda kile kilichotokea.

Tukirudi nyuma kuupitia uchaguzi huu, kulikuwa na kampeni zilizokumbwa na umwagaji wa damu, ambapo vikosi vya usalama nchini humo vilitumia nguvu kupita kiasi kuwabana wapinzani.

Watu wasiopungua 30 waliripotiwa kuuawa katika mji mkuu Kampala, baada ya kutiwa mbaroni kiongozi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi.

Kampeni za uchaguzi uliomalizika, ziligubikwa na kamata kamata ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao, pamoja na kutatizwa kwa shughuli zao za kampeni mara kadhaa na vyombo vya usalama.

Pia Uganda ilifunga huduma ya intaneti wakati wa uchaguzi, ambapo wananchi wa nchi hiyo walikuwa mbali na ulimwenguni na pia ulimwengu ulishindwa kufuatilia kile kilichokuwa kikiendelea wakati wa uchaguzi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Bobi Wine alieleza kwamba nyumba yake imezingirwa na vikosi vya usalama, huku waandishi wa habari na wanasiasa wa upande wake wakizuiwa kuonana naye.

Mgombea huyo aliendesha kampeni zake kwa kuvaa kizibao na kofia ngumu kwa ajili ya kuzuia risasi, ambapo mara nyingi vikosi vya usalama vilikuwa vikikabiliana na wafusi wake.

Wakati wa kampeni, washabiki na baadhi ya viongozi kwenye chama chake kadhaa kuuwawa. Wine alihofia usalama wake wakati wote akiendesha shughuli za kampeni.

Uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao umetatizwa mara kadhaa kwa matukio ya waandishi kushambuliwa wakati wakifanya majukumu yao katika kampeni, kiasi cha wengine kulazwa hospitali wakiwa katika hali mbaya.

Ugonjwa wa corona ulitumika pia kama silaha dhidi ya harakati za upinzani, mikusanyiko ya chama tawala ilikuwa halali, lakini baadhi ya mikusanyiko ya upinzani ilikuwa hairuhusiwi kwa sababu ya corona, ulikuwa ni undumilakuwili wa wazi wazi.

Linalotia shaka zaidi ni kwamba, uchaguzi wenye mlolongo wa matukio yasiyo rafiki kwa mfumo wa kidemokrasia, yataendelea hadi lini katika taifa lenye miaka 58 tangu kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni?

Bado Uganda kama yalivyo baadhi ya mataifa mengine ya Afrika iko katika demokrasia yenye utata mwingi. Upo uhuru wa watu kuchagua viongozi wao, lakini uhuru huo unapita katika misukosuko mingi.

Kinachosemwa na upande wa utawala juu ya uhuru na demokrasia katika siasa, sicho kinachoonekana wakati wa kampeni na uchaguzi. Kuna hadithi tofauti inayoakisi kukosekana usawa kati ya chama tawala na upinzani katika medani ya kisiasa.

Vyombo vya usalama vilidhihirisha kukandamiza upinzani na kusimama na chama tawala. Vilijiingiza katika mizozo kiasi cha baadhi ya maofisa kuonekana katika kamera za wanahabari, wakivutana magwanda wao kwa wao.

Mazingira ya uchaguzi yanaacha swali, kuhusu kilichotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya taifa hilo, ndicho kweli kilichoamuliwa na wananchi katika masanduku ya kura.

Lisilohitaji mjadala ni kuwa, Museveni ataiongoza tena Uganda huku kukiwa kumedhihirika kundi kubwa la vijana ambalo halivutiwi tena na utawala wake, huku wakilalamikia umasikini na ukosefu wa ajira.

Bobi Wine anayo nafasi ya kwenda mahakamani, ingawa matarajio ya wengi mahakama haitokuja na maamuzi ya kupindua matokeo hayo, wapo wanaotilia shaka pia, uhuru wa mahakama hiyo.

Kizza Besigye, aliyekuwa mgombea wa urais katika chaguzi zilizopita. Alikimbilia mahakamani mara kadhaa kupinga ushindi wa Museveni, lakini mahakama haikuwahi kubatilisha kilichohalalishwa na tume.

Kwa kuzingatia historia hiyo, Yoweri Mseveni ana nafasi isiyo na shaka ya kuendelea kuitawala Uganda kwa miaka mengine mitano au zaidi.

Yumkini ndoto ya mpiganaji huyo wa zamani wa msituni mwenye miaka 76, ni kuendelea kuiongoza Uganda hadi pale afya yake itakapo mlazimisha kupumzika au atakapolazimishwa kupumzika.

Bobi Wine bado ana nafasi na muda wa kutosha kuendelea kuwepo katika siasa za Uganda. Ushawishi wake ni mkubwa, na umri unaendelea kumruhusu hata kupambana tena baada ya miaka mitano.

Ingawa kizingiti kikubwa ni kukosekana kwa uwanja safi wa kisiasa hasa kwa upinzani. Na hilo ndilo jambo kubwa anapaswa kulipigania katika hii miaka mitano, kabla ya kurudi tena katika ulingo kupambana na yeyote yule.