Hemed kuzishuhudia Yanga,Jamhuri

NA MWAJUMA JUMA

PAZIA la michuano ya kombe la mapinduzi linafunguliwa leo visiwani Zanzibar kwa kupigwa michezo miwili ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Hemed  Suleiman.

Michuano hiyo itashirikisha timu tisa ambapo kwa mujibu wa ratiba hiyo wakati wa saa 10:00 za jioni Mtibwa ambao ni mabingwa watetezi watacheza na Chipukizi.

Mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo utakuwa ni kati ya Yanga na Jamhuri ambao utachezwa  saa 2:00 usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Katibu wa Kamati ya Mashindano Imane Osmond Duwe alisema  maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika kwa asilimia 100.

“Kimsingi yale mambo yote muhimu ambayo yanahitajika katika mashindano yamekamilika kwa asilimia 100 na sasa tunasubiri siku ifike tu ili mashindano yaanze rasmi”, alisema.

Aidha alisema  katika mashindano hayo wasanii mbali mbali wa Zanzibar na Tanzania Bara watakuwepo.

Aliwataja wasanii hao ni Ali Kiba, Zuchu, Mboso, JUX na AT, sarakasi na msanii kijana anaepiga violini kwa uwezo mkubwa Sana.

Alisema katika mechi rasmi ya ufunguzi msanii Ali Kiba atafanya onyesho la moja kwa moja pamoja na Sanaa za sarakasi, muziki lakini, beni na ngoma za asili.

Aidha alisema  watoto wenye vipaji kutoka akademi ya soka Zanzibar nao wataonyesha vipaji vyao uwanjani.

Hata hivyo alisema watu maarufu kama mtangazaji machachari Salama Jabir na Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, pamoja na kamati ya uhamasishaji ambayo inaongozwa na Taufiq Turkey ambae ni mbunge wa Jimbo la Mpendae.

Katika michuano hiyo bingwa anatarajiwa kupata kombe, medali za dhahabu  na  shilingi milioni 15 na mshindi wa pili atapewa shilingi milioni 10, medali za fedha na kikombe.

Wakati huo huo kamati ya mashindano imefanya mabadiliko madogo ya ratiba pamoja na viingilio vya uwanjani.

Katibu huyo alisema mabadiliko ya ratiba yamefanywa kwa mechi ya Simba ambayo awali ilipangwa kuchezwa Januari 7, mwaka huu.

Simba ambayo inashiriki ligi ya mabingwa Afrika awali ilipangwa kucheza mchezo wake huo wa kimataifa Januari 5 lakini badala yake watacheza Januari 6 mwaka huu hali iliyopelekea kufanyika mabadiliko ya ratiba hiyo na kupangwa  kuchezwa Januari 8, mwaka huu.

Aidha alisema  mechi namba tano kati ya Azam na Mlandege itachezwa Januari 7 mwaka huu, saa 2:00 usiku.

Kuhusu viingilio alisema kamati baada ya kupitia maoni ya wadau wao umefanya mabadiliko ya viingilio ambapo tiketi zitauzwa shilingi 3000 kwa jukwaa la Urusi na Mzunguuko wake badala ya shilingi 2000.

Alisema  tiketi hiyo mshabiki ataweza kuangalia mechi zote mbili za jioni na usiku.

“Tumeona umuhimu wa thamani ya pesa ambayo mtu atatoa katika kukata tiketi hivyo wataweza kuangalia mechi mbili kwa siku moja tutaandaa utaratibu kwa wale ambao wanaotaka kutoka kwenda kusali na kula”, alisema.