WASHINGTON, MAREKANI

SIKU moja baada ya Rais mteule wa Marekani Joe Biden kupata ushindi mpya, ambapo chama chake cha Democratic kilitabiriwa ushindi katika uchaguzi wa marudio wa nafasi mbili za seneti jimboni Georgia, jambo hilo lilisababisha wafuasi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuwa na hasira kali na kusababisha machafuko kwa kuandamana huku wakiimba, “Tunamtaka Trump”.

Wafuasi hao wa Trump wamevuka mipaka ya usalama iliyowekwa na kusimama kandokando ya bunge huko Washington, wakati wabunge wanakutana kumuidhinisha Rais mteule Joe Biden kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.

Kitendo hicho kimesababisha viongozi wengi duniani kutoa wito wa amani na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya utulivu, huku wakieleza kuwa uvamizi uliotokea ni jambo la kutia aibu.

Rais wa zamani wa Marekani Barak Obama ametoa taarifa yenye lugha kali, kwa kusema kitendo hicho kitakumbukwa katika historia ya nchi hiyo, ambapo ghasia hizo zimechochewa na Rais wa sasa kwa uongo wake usio na msingi kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais, kuwa ni fedheha na aibu.

Obama ameashiria hujuma ya kipropaganda ya wanachama wa Rarepublican dhidi ya ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana na kutahadharisha kuwa, wafuasi hao wanakabiliana na njia mbili, ambazo ni kuendeleza njia hii na kuchochea moto wa hitilafu, au kuchagua haki na ukweli.

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amewataja wafuasi wa Trump kuwa ni magaidi wa ndani ya nchi ambao wanapaswa kuwajibishwa.   

Akizungumzia tukio hilo Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza ameonesha mzimamo wake kwa kulaani vikali na kusema kuwa tukio hilo la kuvamiwa Congresi ya Marekani ni fedheha kubwa ulimwenguni.

Aidha ameendelea kwa kuandika katika ukurasa wake wa ‘twitter’ kwamba suala la kukabidhi madaraka huko Marekani linapaswa kufanyika kwa amani na utulivu. 

Nae Jens Stoltenberg Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) ameandika katika ukurasa wake wa ‘twitter’ kwamba, ” Matokeo ya uchaguzi wa kidemokrasia wa chini Marekani yanapasa kuheshimiwa.”

Akizungumzia ghasia na machafuko hayo huko, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas pia amewatolea wito Trump na wafuasi wake waheshimu uamuzi wa wapiga kura wa Marekani na kutokanyaga demokrasia.

Aliongeza kuwa, maadui wa demokrasia watafurahishwa na matukio kama haya yasiyoweza kutarajiwa.

Nae Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, alilaani kitendo hicho na kusema kuwa “ni aibu,nchi kama  Marekani inasimamia demokrasia kote duniani na ni muhimu sana kuwa na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani na wenye mpangilio,” ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alieleza wasiwasi wake kuhusu matukio yanayojiri huko Marekani ametaka kuhitimishwa ghasia nchini humo.

Viongozi wengine wa kisiasa nchini Marekani wamekosoa ghasia hizo huku kiongozi wa upinzani Sir Keir Starmer akitaja kitendo hicho kama “uvamizi wa moja kwa moja wa demokrasia”.

Wazriri wa kwanza wa Scotland Nicola Sturgeon ameandika kuwa kinachotokea bungeni “kinatia hofu mno”.

Nae Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez amesema, “Nina imani na demokrasia ya Marekani,  uongozi wa Rais mpya Joe Biden utakabiliana na kipindi hiki kigumu, kuunganisha watu wa Marekani.”

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amelaani kitendo hicho na kusema ni “uvamizi mbaya dhidi ya demokrasia”, huku mwenzake wa Ujerumani, Heiko Maas, akisema bwana Trump na wafuasi wake “lazima wakubali uamuzi wa wapiga kura wa Marekani na waache kutatiza demokrasia”.

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema kuwa aliiamini sana Marekani katika kuhakikisha ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani kwa Bwana Biden.

Nae Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema ana matarajio makubwa ya ushirikiano na chama cha Democrat.

Akisisitiza usalama wa nchi hiyo ya Marekani Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg aliungana na wale waliosema matokeo ya uchaguzi ni lazima yaheshimiwe.

Akizungumzia Jambo hilo lilozua mjadala duniani kote, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema raia wake “wamehuzunishwa sana na kitendo hicho cha uvamizi wa demokrasia”.

Trump aliekataa kukubali kuwa ameshindwa katika uchaguzi wa Novemba 3 na kudai mara kadhaa kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura bila kutoa ushahidi wowote aliwataka wafuasi wake kukusanyika mbele ya jengo la Kongresi mjini Washington.

Jambo lililopelekea waandamanaji hao kufika katika majengo ya bunge kutoka kwenye mkutano uliopewa jina la “Save America Rally”, ambapo Trump aliwataka wafuasi wake kuunga mkono wabunge wanaopinga kuidhinishwa kwa Biden kama mshindi.

Polisi walijibu maandamano hayo kwa kutumia bunduki na mabomu ya machozi wakati mamia ya waandamanaji walipovamia na kutaka kulilalazimisha bunge kubatilisha ushindi wa Biden dhidi ya rais Donald Trump, ambapo muda mfupi baada ya warepublican wenzake na Trump kuanzisha juhudi za dakika za mwisho ili kubatilisha  ushindi wa Joe Biden.

Ghasia hizo zilisababisha kuhairishwa kwa kikao hicho baada ya wafuasi hao wa Trump kuvamia ndani ya jengo hilo, huku wabunge nao wakisindikizwa kutoka bungeni humo kwa msaada wa polisi.  

Taarifa zilieleza kuwa Makamu wa Rais Mike Pence, aliyekua anaongoza kikao hicho aliondolewa mara moja na walinzi wa usalama wa Rais kupitia njia ya chini kwa chini za jengo la bunge.

Utaratibu wa kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa Rais kawaida ni sherehe inayofanyika ndani ya bunge kama hatua ya mwisho ya kuidhinisha rasmi matokeo ya Wajumbe wa uchaguzi walompatia ushindi Biden hapo Disemba 14 lakini utaratibu huo ulipingwa na wabunge wachache wa chama cha Republican.

Ripoti zinaeleza kuwa watu wasiopungua wanne wameuawa katika ghasia na machafuko hayo.

Bunge la Marekani limepiga kura ya kumuidhinisha rais mteule Joe biden kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliopita.

Bunge hilo lilimuidhinisha Biden kwa kura 282 huku wabunge 138 wakipiga kura ya kupinga matokeo ya jimbo la Pennsylvania.

Ikiwa Democrat itashinda viti vyote, Biden atakuwa na udhibiti wa bunge la Seneti na hilo litasaidia kupitisha ajenda zake baada ya kuapishwa rasmi kama Rais wa Marekani ifikapo Januari 20.