NA NAFISA MADAI

WIZARA ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, imeshauriwa kazi za utiaji viraka kwenye barabara mbalimbali za mjini ifanyike wakati wa usiku ili kuondosha msongamano kazi hiyo inapofanyika mchana hususani muda wa kwenda na kutoka kazini.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati, Panya Ali Abdallah mara tu baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi katika Mamlaka ya Wakala wa Barabara Zanzibar.

Panya alisema ni vyema kazi za uzibaji viraka ikapewa kipaumbele zaidi kwa kufanyika wakati wa usiku kutokana na muda wa mchana kuwa mambo mengi.

Mwenyekiti huyo aliutaka wakala huo kudhibiti gari za mizigo kwa kuhakikisha uzito wa mizigo inayopakiwa inakwendana na uwezo wa barabara.

Aliitaka wizara kupitia wakala huo kuandaa mpango maalum wa kuweka alama za uhifadhi wa njia kabla ya ujenzi wa barabara ili kuepusha uvamizi wa maeneo hayo unaofanywa na baadhi ya wananchi.

Panya alieleza masikitiko yake kwa baadhi ya taasisi za serikali kuvunja barabara pale tu zinapojengwa kwa kupitisha miundombinu ambapo alisema ni vyema kwa taasisi hizo kufanya mawasiliano mapema ili kunusuru gharama zikazojitokeza.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa wakala wa barabara, Faudhia Haji Sinde akisoma ripoti hiyo ya utekelezaji kwa kamati hiyo, alisema wakala una jukumu la kujenga barabara mpya, kutunza na kusimamia mtandao wa barabara.

Alisema hadi sasa mtandao huo una kilomita 1, 328.52 kati ya urefu huo kilomita 834.11zimejengwa kwa lami kwa visiwa vyote vya Unguja na Pemba.

Naye katibu mkuu wa wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa kamati hiyo, alisema wizara kupitia wakala wa barabara imebaini kuna changamoto kubwa za matumizi ya barabara.

Alisema barabara nyingi kuwa na mashimo kunatokana na ukosefu wa elimu kwa watumiaji ambapo alifahamisha kuwa sumu kubwa ya kuharibika barabara ni mafuta yanayotoka kwenye gari.

Wajumbe wa kamati hiyo kwa upande wao walipata nafasi ya kuchangia na kushauri baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuleta maendelea ya nchi.

Katika hatua nyengine kamati hiyo ilipokea taarifa ya utekelezaji kutoka katika Shirika la Bandari iliyosomwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu Juma Haji Juma, ambapo alisema shirika limeweza kukusanya fedha nyingi kwa kipindi hiki kuliko kipindi kilichopita.