NA HAFSA GOLO

VIJANA wameshauriwa kufata  tabia njema,uadilifu,pamoja na  kuthamini uzalendo wao kwani itasaidia kuwajenga katika misingi na maadili mazuri katika maisha ya kila siku. 

Mwakilishi wa jimbo la Donge, Dk. Khalid Salum Mohamed,  alitoa ushauri huo alipokua akizungumza na vijana wa jimbo hilo,katika ziara za kuwashukuru wapiga kura kwa kuichagua CCM kwa kiwango kikubwa cha kura kuanzia ngazi za jimbo hadi taifa.

Dk.Khalid  alisema endapo vijana watakuwa na moyo wa  kuthamini uzalendo wao,kusimamia  misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964 iliyoasisiwa na Jamadari Mzee Abeid Amani Karume itawasaidia kuwajengea mazingira bora endelevu na taifa lenye kujivunia nguvu kazi imara. 

Alisema kwamba kuwa na  tabia njema na maadili mazuri kwa vijana ni miongoni mwa njia inayosaidia kuepukana na  itikadi zenye chuki na ubaguzi  miongoni mwao na hatimae nchi  itakuwa na viongozi  imara ambao wanajali  taifa lao.

Hivyo aliwataka vijana hao kuweka kipaumbele  cha kupinga vita dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote,  badala yake wazingatie haki na usawa katika mwenendo wa maisha ya kila siku.

Alisema mfumo huo utasaidia  kwa  vijana hao kudumisha amani na utulivu sambamba na kuibua fikra sahihi za uimarishaji wa maendeleo katika maeneo wanayoishi na taifa kwa jumla.

“Huu sio wakati wa siasa za chuki na ubaguzi nakuombeni dumisheni umoja na mshikamano kwani nchi inahitaji maendeleo na sio vurugu “,alisema.

Pamoja na hayo Dk.Khalid,aliwataka vijana hao kuiunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Huusein Ali Mwinyi katika kupambana na rushwa,udhalilishaji na matumizi mabaya ya madaraka.

Nae Katibu wa Chama cha Mapinduzi Jimbo la Donge Haji Boko,alisifu juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na viongozi wa jimbo hilo katika kuelimisha vijana juu ya mfumo mzuri wa kuishi.

Alisema iwapo vijana watajengwa katika maadili mema itasaidia kitaifa kuwa na viongozi wema wa baadae sambamba na ongezeko la nguvu kazi ya maendeleo.

Aidha alisema nchi nyingi duniani vijana wake wamekuwa na utaratibu mzuri wa mfumo wa maisha ikiwa ni pamoja na kusimamia uzalendo na miongozo ya nchi zao hivyo Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa  nchi hizo inapaswa kuhakikisha vijana wake wanakuwa na misingi mema.

Kwa upande wa vijana hao walipongeza juhudi za viongozi hao katika suala zima la kuhimiza mwendo bora wa maisha, ikiwa ni sambamba na kuheshimu uzalendo na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao.