NA HAFSA GOLO

KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini  Kaskazini B Unguja, Mula Othman Zubeir, amewataka vijana kuilewa vyema historia ya nchi yao, kwani itasaidia kufikia azma ya malengo ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.

Alieleza hayo wakati alipokua akizungumza na vijana kuhusu Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliofanyika Mahonda  Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema vijana iwapo watasimamia ipasavyo misingi yenye kujenga na kuendeleza tamaduni na historia ya nchi yao, bila ya shaka  itasaidia kuleta hamasa na uchapakazi wenye maslahi mapana nchini sambamba na ushiriki wa miradi ya maendeleo inayoekezwa bila ya shuruti.

Mula alisema, lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ni kulinda, kuheshimu utu wa Muafrika, upatikanaji wa haki na wajibu katika huduma muhimu za mahitaji ya binaadamu ikiwemo ya kiuchumi na kijamii.

“Zanzibar mara baada ya Mapinduzi miradi mingi ilijengwa kwa mashirikiano ya serikali na wananchi wake kutokana na hamasa na mwamko wa malengo ya viongozi wao”,alisema.