NA ABDI SULEIMAN
MBUNGE wa viti maalumu wanawake mkoa wa kaskazini Pemba, Asiya Sharif Omar, amewataka vijana kuendelea kuyajali na kuyathamini mapinduzi kwani ndio yaliyotoa fursa sawa kwa wananchi.
Alisema hayo wakati akizungumza na wananchi, wanaCCM na wazee wa Jojo wilaya ya Wete, baada ya uwekaji wa jiwe la msingi maskani ya CCM ya Dk. Ali Mohamed Shein iliyoko Jojo.
Alisema mapinduzi ya 1964 yametoa fusa zote kwa wazanzibari, ikiwemo elimu bure, matibabu bure, hivyo vijana wanapaswa kumuenzi marehemu mzee karume kwa vitendo.
“Hatuna budi kuwashukuru viongozi wetu wa nchi Rais Dk.Hussein Mwinyi na Rais Dk.John Magufuli, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zao walizoziweka kwa wananchi,” alisema.
Hata hivyo, aliwataka vijana kujiandaa kuupokea uchumi wa buluu kwa vitendo, kwani viwanda vinatarajiwa kujengwa vikiwemo vya uvuvi.
Katibu wa CCM jimbo la Kojani, Ali Omar Ali, alisema vijana hao sio wa kupanda gari na kushuka bali wameandaliwa na kukomaa kisiasa kwa sasa.
Mohamed Khatib Faki kutoka maskani ya Karume Kruu ya Kambini Kichokochwe, alisema vijana wameanza vizuri kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane, katika kupiga hatua za maendeleo kwa kubuni miradi ya maendeleo.
Akisoma risala ya maskani hiyo, Bishara Suleiman Ali alisema ujenzi huo ulianza mwaka 2018 na kwa sasa maskani hiyo ina vijana 50.
Alisema jumla ya shilingi milioni 7.5 zimetumika katika ujenzi wa maskani hiyo.