NA SAID ABRAHAMAN
MKUU wa JKU Pemba, Kanali Machano Kombo Khamis, amewataka vijana kuyatumia vizuri mafunzo waliyoyapata ili wajiendelezE kimaisha.
Alisema lengo la serikali kuwapeleka vijana hao katika kambi za JKU sio adhabu bali ni kujenga taifa lao na kupata stadi za maisha.
Aliyasema hayo ofisi kuu ya JKU Wawi wakati
akifunga mafunzo ya mkupuo wa 065 ya vijana wa
JKU.
Aliwaeleza vijana hao kuwa kujiunga kwao na JKU
ilikuwa sio ajira bali ni kujenga taifa
na kuwa wazalendo na nchi yao, hivyo aliwataka vijana kuyatumia vizuri.
Aliwataka vijana hao kujiingiza katika vikundi vya ushirika ili waweze kujiendesha kimaisha na kuacha kutegemea ajira kutoka serikalini.
Alisema endapo vijana hao watajikusanya na kuunda vikundi vya ushirika, JKU liko tayari kuwasaidia kwa kuwapatia taaluma itakayowawezesha kuwasaidia.
“Ninachoamini mmejifunza mambo mengi ya ujasiriamali wakati mlipokuwa katika mafunzo yenu, lililobakia kwenu mkajiendeleze zaidi kwani serikali ya awamu ya nane inasisitiza vijana kufanya kazi,” alisema.
Mapema Kanali Machano aliwanasihi vijana hao
kutojiingiza katika masuala
ya utumiaji wa dawa za kulevya kwani ni hatari kwa maisha yao.
Aliwataka vijana hao kujiepusha na vitendo
vya udhalilishaji kwani vinatia doa nchi.
Mkuu wa utawala JKU Pemba, Meja Ramadhani Mkubwa,
aliwataka vijana hao kuwa kioo kwa jamii
na kuwa tofauti na vijana wengine.
“Leo mnamaliza mafunzo yenu na mnarudi nyumbani, ninalowasisitiza kaweni mfano nzuri kwa vijana wenzenu na kwa jamii,”alisema.
Meja Said Khamis Omar aliwasisitiza, vijana
kujiepusha na vigenge
ambavyo havikubaliki ili kutojiingiza katika matatizo.
Akisoma risala ya wahitimu hao, Luteni Usu Omar
Ramadhan Mtipura, alieleza kuwa
changamoto kubwa ambazo walikabiliana nazo vijana hao
wakati wakiwa katika mafunzo yao ni pamoja na
ukosefu wa mahanga ya kulala pamoja na
vitanda vyake.
Hata hivyo, walipendekeza kuwepo kwa utaratibu
mzuri wa kupata mafunzo pamoja na
kuwakusanya sehemu moja tu kama ilivyokuwa hapo awali.