NA LAILA KEIS

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) limekamilisha matengenezo ya kufikisha umeme katika kijiji cha Kibumbwi, ikiwa ni moja kati ya sera za serikali ya kuhakikisha vijiji vyote vilokuwa havina umeme vinapatiwa huduma hiyo, ili kutimiza azma ya kuleta maendeleo kwa kila mwananchi.

Meneja mkuu Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Hassan Ali Mbarouk, aliyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya matengenezo hayo, katika kijiji hicho kilichopo Mkoa wa Kaskazini, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Alisema ZECO imetimiza ahadi yake ya kufikisha umeme katika kijiji hicho, ambayo iliahidi kukamilika kwa matengenezo ya umeme huo ndani ya miezi mitatu, lakini kwa kulipa umuhimu jambo hilo wamelifanikisha ndani ya mwezi mmoja.

“Tumeweza kuleta umeme kwa kujenga njia kubwa ya umeme ya mkondo wa kv 33 yenye urefu wa kilomita moja na nusu, vilevile tumesambaza umeme mdogo wenye masafa ya kilomita mbili, pamoja na kuweka transfoma yenye uwezo wa Kva 50” alisema.

Akizungumzia gharama za kufanikisha zoezi hilo, alisema takribani ya shilingi milioni mia moja zilitumia katika kukamilisha zoezi hilo, ambazo zote zimetolewa na serikali kupitia ZECO.

Sambamba na hilo, aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuitumia fursa hiyo iliyoletwa na serikali kwa kuunga umeme huo majumbani kwao, ili kujiletea maendeleo.

“Ninawaomba wananchi kwamba huduma imeshafika katika kijiji chao, hivyo kilichobaki ni wao kuitumia huduma hii, kwani haitokuwa vyema kwamba wameomba umeme halafu ukakaa bila ya wao kuutumia” alisisitiza.

Aliongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa punguzo la asilimia 50 la umeme, kutoka 400,000 hadi 200,000, lakini kwakuwapa kipaombele wanakijiji hicho ZECO imewarahisishia kwa kuwaruhusu walipe 100,000 kwanza na zilizobaki watalipa kidogo kidogo, ili kuwasaidia katika changamoto ya gharama.

Akizungumzia mikakati ya kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wanakijiji hao ipasavyo, Meneja Mawasiliano na huduma za wateja Salum Abdallah Hassan, alisema, ZECO imeandaa zoezi maalumu la kutoa elimu ili kufanikisha matumizi bora ya umeme.

“Ni vyema kwa wanakijiji wakajua matumizi ya umeme na athari zake, kwani kama inavyojulikana kuwa umeme ni hatari, hivyo tunafika maeneo mapya ili iwe rahisi kwa wanakijiji nao kuweza kuuliza kwa walilokua hawalijui kuhusiana na umeme” alieleza Meneja Salum.

Nae mmoja wa wanakijiji hicho, Kurwa Hussein, aliishukuru serikali kupitia ZECO kwa kuleta umeme ambao kilikua kilio chao cha muda mrefu, kwani walipata tabu na kukosa huduma nyingi za muhimu ambazo zinahitaji umeme kama vile maji, ambapo visima vilikauka kwa muda mrefu tangu kuharibika umeme wa jua waliokua wakitumia.

Aidha Kurwa aliwataka wanakijiji wenzake kujitokeza kwa wingi kuunga umeme huo, ambao serikali imegharamika katika kufanikisha kupeleka huduma hiyo kwa haraka zaidi ya matarajio yao.