NA KHAMISUU ABDALLAH

SAMPULI ya vijiwe tisa alivyodaiwa kupatikana navyo Khamis Said Hamad (24) mkaazi wa Magogoni, vimemsababishia kufikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Asya Abdalla Ali na kusomewa shitaka na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya DPP, Soud Said.

Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuapatikana na dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009 sheria za Zanzibar.

Mwendesha Mashitaka Soud alidai kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya sapuli ya vijiwe tisa aina ya heroini, vyenye uzito wa gramu 0.9243 zikiwa ni kiwango kidogo, ambazo zilikuwemo katika kifurushi cha karatasi ya mng’aro kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Khamis alidaiwa kuwa, alipatikana na kosa hilo Julai 16 mwaka huu saa 5:00 asubuhi huko Magogoni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mahakama ilikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Januari 20 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Pia Hakimu Asya alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi na kuwasilisha vitambulisho vinavyotambulika na serikali.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.