NA MWAJUMA JUMA

MIAMBA minne ya soka inayoshiriki ligi daraja la pili wilaya ya Mjini ilitoka kidedea katika michezo yao iliyochezwa juzi katika viwanja vya Mao Zedong.

Miamba hiyo ni New Boko ambayo ilicheza uwanja Mao Zedong B saa 7:30 na kuifunga West Coast bao 1-0 lililofungwa na Seif Issa dakika ya 19 na saa 10:00 uwanjani hapo Amani Fresh ikaifunga FC Dira kwa idadi kama hiyo ya bao lililowekwa kimiyani na Omar Nassor dakika ya saba.

Aidha katika uwanja wa Mao Zedong A saa 7:30 University ilicheza na Ajax na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 mabao yake yalifungwa na Saleh Masoud dakika ya tisa na 41, Said Hamad dakika ya 31 na Asaa Hamad dakika ya 52.

Kwa upande wa Ajax mabao yake yalifungwa na Hashir Ramadhan dakika ya 20, Yussuf Juma Ali dakika ya 33 na Nasir Mzee dakika ya 68.

Majira ya saa 10:00 uwanjani hapo timu ya Maruhubi iliwakaribisha wanagenzi wa ligi hiyo timu ya Jamaika kwa kuwafunga mabao 2-0, ambayo yalifungwa na Omar Dhamir dakika ya 16 na Mustafa Ramtula dakkika ya 78.

Ligi hiyo leo inatarajiwa kuendelea tena kwa kupigwa michezo miwili ambapo katika uwanja wa Mao Zedong A Muembemakumbi itacheza na Elhila na Mao Zedong B, Danger itapambana na Polling Land, michezo ambayo yote itachezwa wakati was aa 7:30.