NA HAJI NASSOR

VYAMA vya ushirika kisiwani hapa vimeshauariwa kujiunga na taasisi ya fedha ya Faraja Union Ltd, ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

Hayo yalielezwa na aliyekuwa Ofisa Mdhamini Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Hakim Vuia Shein, alipokuwa akifungua kongamano la vyama vya ushirika, lililoandaliwa na taasisi ya Faraja Union Ltd na kufanyika ukumbi wa baraza la mji Chake Chake.

Alisema, zipo baadhi ya benki zinatoza kiwango kikubwa cha riba, jambo ambalo linazikwaza sacos ikiwa ni pamoja na kushindwa kurejesha mikopo.

Alisema, jambo hilo halipo ndani ya taasisi ya Faraja Union Ltd, hivyo ni wakati wa vyama vya ushirika na sacos kujiunga ili kutimiza ndoto zao.

Alisema vyama vingi vya ushirika vina hali duni kiuchumi, hivyo vinapoomba mkopo na kisha kuweka masharti magumu ikiwa ni pamoja na riba kubwa, hudhoofika na kupoteza malengo yao.

Hivyo, alisema kama vipo vyama ambavyo hadi sasa havijajiunga na taasisi hiyo wakati ndio huu ili kutimiza malengo yao.

“Ni kweli kuwa vyama vya ushirika vinakabiliwa na changamoto kubwa katika kuomba mikopo kwa kuwepo masharti magumu, ikiambatana na riba kubwa wakati wanapoirejesha,”alisema.