NA TATU MAKAME

WAANDISHI wa habari wa vyombo mbali mbali wamesema uvamizi wa fani ya habari kwa wasiokuwa na sifa pamoja na maadili ya kazi hiyo kumepelekea wananchi kutokuwa na imani na baadhi ya vyombo vya habari vinavyotoa na kurusha habari katika jamii.

Wakizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari huko Kidongochekundu Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, juu ya mafunzo ya kujenga amani ya nchi waandishi hao walisema kumekuwa na matumizi mabaya kwa vyombo vya habari.

Walisema hivi sasa waandishi wengi wamekuwa wakishindwa  kutofuatilia kwa undani habari wanazotoa katika taasisi zao na kupelekea kutoa taarifa zisizothibitishwa ambazo zinaweza kuleta migogoro kwa jamii.

Walisema hali hiyo imekuwa ikishusha hadhi ya fani ya habari na kuonekana waandishi hawazingatii maadili wanayofundishwa.

Akitoa mafunzo juu ya wajibu wa wanahabari mkufunzi, Mohammed Hafidh aliwataka waandishi kuandika kwa kuzingatia umuhimu wa habari na kuchuja yasiyofaa katika habari zao kabla ya kurusha katika vyombo vyao ili kuepusha hamasa mbaya kwa wananchi ambazo zinaweza kuharibu Amani.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na jumuiya ya vijana zanzibar youth forum kwa ufadhili wa foundation for civil society kupitia mradi wa miaka mitatu kwa lengo la kujenga umoja miongoni mwa wananchi kupitia vyombo vya habari.