MAPUTO, MSUMBIJI

MAMIA ya wakazi wa wilaya ya Buzi nchini Msumbiji wanasubiri kuondolewa katika eneo la kituo cha Guara Guara baada ya nyumba zao kuharibiwa na kimbunga Eloise.

Baadhi ya wakaazi katika eneo hilo walieleza kuwa hadi jana walikuwa kwenye msururu kwa siku tatu wakisubiri kusaidiwa kuondoka kutokana na athari za kimbunga hicho.

Taasisi ya kitaifa inayoshughulikia udhibiti wa majanga nchini Msumbuji (INGD), ilibainisha kuwa operesheni zinaendelea na kwamba zinafanywa taratibu ili kuhakikisha usalama wa kila mmoja.

Baadhi ya wale walioondolewa wamepelekwa kwenye makaazi binafsi huku wengine wakipelekwa kwenye vituo vya makaazi.

Mkuu wa shirika la INGD, Luisa Meque alisema watu wanapaswa kuondoka kutoka kwenye maeneo hatari mapema kuepuka athari zaidi za kimbunga hicho.

INGD ilisema watu wengi walipuuza tahadhari na wale walioondolewa kwanza walikwenda kituo cha Guara Guara baada ya nguvu kutumika.Familia nyingi zilimewasili Guara Guara, na haijulikani itawachukua muda gani kuondolewa.