NA NASRA MANZI

NAIBU Katibu Mkuu Kamati ya Olimpiki Tanzania TOC Suleiman Mahmoud Jabir amewataka wachezaji wa mpira wa mikono kujenga nidhamu kwenye michezo ili kufikia malengo waliokusudia.

Jabir alitoa kauli hiyo wakati akifungua mashindano ya kombe la mapinduzi ya miaka 57 hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa Migombani jeshini.

Alisema  nidhamu katika michezo ndio njia pekee itakayowasaidia kupata mafanikio, pamoja na kupiga hatua za kimaendeleo.

Pia alikipongeza Chama cha Mpira wa Mikono Zanzibar (ZAHA) kwa uhudi zake za kufanya mashindano kwa kushirikisha timu za Tanzania bara ,jambo ambalo litaleta ushindani wa soka ,pamoja na kujenga umoja na udugu miongoni mwao.

Aidha alikipongeza chama hicho na kile cha Tanzania bara  (TAHA) , kwa kushirikiana pamoja katika kuhakikisha mchezo huo unaimarika.

Pia aliwataka wanamichezo hao kutumia michezo kujiepusha na viashiria ambavyo havitawaletea mafanikio pamoja na kujikinga na maradhi ya ukimwi.

Katibu wa chama cha mpira wa mikono Zanzibar ZAHA Mussa Abdulrabi alisema bado wanachangamoto kwa baadhi ya wanawake kushiriki mchezo huo,hivyo chama kitaendelea kutoa taaluma ili kuzidi kupatikana vipaji .