BEIJING, CHINA

WAFANYAKAZI waliokamatwa katika mgodi wa dhahabu wa China kwa zaidi ya siku tisa wamepokea vifaa vya matibabu na chakula, pamoja na bandeji na blanketi.

Vyombo vya habari vya Serikali vilisema,jumla ya wafanyakazi 22 walinasa katika mgodi wa Hushan, katika mkoa wa Shandong, baada ya mripuko Januari 10.

Baada ya wiki moja iligundulika kwamba watu 12 kati yao  bado walikuwa hai wakati ilipotumwa barua kutoka mgodini.

Waokoaji walichimba njia tatu zaidi, kulingana na ramani ya uokoaji iliyochapishwa kwenye akaunti rasmi ya serikali ya Yantai Weibo, toleo la Kichina la Twitter.

Zaidi ya watu 300 wanahusika katika juhudi za uokoaji na wachimbaji na mashine ziko kwenye tovuti lakini timu hizo zilionya kuwa itakuwa ngumu sana kuwatoa wachimbaji kutoka lango la handaki.

Shirika rasmi la habari la Xinhua limesema wachimbaji hao waliomba soseji na kachumbari pamoja na uji lakini wataalam wa matibabu walisema hawapaswi kula chakula kigumu wakiwa wamepata nguvu tu.

Hata hivyo, gazeti la serikali la People’s Daily limesema mfanyakazi mmoja alikuwa katika hali ya kukosa fahamu na hali mbaya, baada ya kupata jeraha la kichwa katika mripuko huo.

Mfanyakazi mmoja zaidi amekuwa katika sehemu nyengine ya mgodi, wakati wengine kumi bado hawajulikani waliko.