NA MWANDISHI WETU

Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuendeleza ushirikiano na serikali ili kuhimiza kasi ya maendeleo ya jamii na uchumi wa Zanzibar.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima Zanzibar (ZNCC) uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni, Zanzibar.

Alisema serikali ya awamu ya nane imefungua milango kwa sekta binafsi ili itoe mchango zaidi katika maendeleo ya nchi hivyo jumuiya hiyo inapaswa kuweka malengo ya kuwabadilisha wajasiriamali wadogowadogo kuwa wazalishaji wa kati.  

Alisema hali hiyo mbali ya kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, itaongeza idadi ya wafanyabiashara na wazalishaji ambao pia wataajiri kwa wananchi wengi zaidi.

“bila shaka wakati umefika kujadilina namna mtakavyoziwewzesha biashara ndogo ndogo kuwa biashara za kati ili kukuza wigo wa biashara na kuongeza mapato ya kodi jambo litakaloongeza uwezo wa serikali kuhudumia jamii,” alieleza.

Aliipongeza jumuiya hiyo kwa kuendelea kuwa kiungo kati ya serikali na wanachama wake jambo lilitoa fursa ya kuwepo kwa ufanisi wa kibiashara kati ya pande mbili hizo.

Aidha Hemed pia alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama wa jumuiya hiyo kufuata sheria zilizopo sambamba na kuendeleza majadiliano na serikali kwa lengo la kuweka utaratibu mzuri wa kibishara.

Awali Mwenyekiti wa mkutano huo, Fatma Khamis Mbarouk alieleza kuridhishwa kwa jumuiya hiyo na kasi ya mashirikiano kati ya sekta binafsi na serikali jambo alilosema litapunguza kwa kiasi kikubwa vikwazo vya kibiashara na uwekezaji nchini.

Alisema ili mafanikio ya haraka yapatikane, lakizi kuwe na mashirikiano yanayonufaisha pande zote mbili na kuahidimkuwa ZNCC itaendelea kusimamia misingi ya majadiliano kati yake na serikali ili kuwa na mwenendo mzuri wa biashara.

“Tutaendeleza mashirkiano na serikali ili dhana ya PPP (Public Private Partnaship) ifanikiwe kwani tumeona mwanga wa matumaini na bila shaka changamoto nyingi za kibiashara, wakulima na wawekezaji zitapatiwa ufumbuzi,” alieleza Fatma ambae pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara wanawake Zanzibar.

Nae mkurugenzi mtendaji wa jumuiya hiyo Ahmad Omar Ahmad alieleza kuwa pamoja na changamoto ya maradhi ya corona, zncc imefanikiwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya majadiliano na serikali kulikopelekea kupunguzwa kwa kodi katika sekta ya utalii na biashara nchini.

Alisema hatua hiyo imeongeza ufanisi katika biashara licha ya kupelekea baadhi ya biashara kufungwa na wananchi kupoteza ajira.

“Tunashukuru katikam kipindi cha maradhi ya corona, serikali iliendelea kuwa pamoja nasi na kuwerka miundombinu iliyosaidia kuzilea baadhi ya biashara kwa kusaidia kupunguza kodi na kuondoa ushuru,” alisema Ahmad.

Katika mkutano huo, agenda 11 ziliwasilishwa ikiwemo ya uchaguzi ambapo wajumbe wa mkutano huo walimchagua aliekuwa Makamu Mwenyekiti ali Suleiman Amour alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ZNCC baada ya kupata kura 74 za ndio na Hassan Mohammed Raza alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti baada ya kupata kura zote 80 zilizopigwa.

Uchaguzi wa nafasi hizo umekuja baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wake Taufiq Salum Turky kujiuzulu wadhfa huo baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu uliopita huku Amour aliekuwa akikaimu nafasi hiyo akijiuzulu ili kugombea Uenyekiti.