NA KHAMISUU ABDALLAH
WAFANYAKAZI wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar wametakiwa kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza ufanisi kazini na maendeleo ya jamii.
Mhariri Mtendaji wa shirika hilo, Yussuf Khamis Yussuf alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo ikiwa ni sehemu ya kuanza kwa awamu mpya ya serikali ya awamu ya nane, uliofanyika katika ofisi za shirika hilo Maisara.
Alisema, kukaa na kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano kutaliwezesha shirika hilo linalochapisha magazeti ya Zanzibar Leo, Zanzibar Mail, Zaspoti na Zanzibar Leo Wanawake kusonga mbele kimaendeleo.
Alifahamisha kuwa ni vyema wafanyakazi wakaweka tofauti zao pembeni na kuishi kama ndugu wanapokuwa kazini ili kuongeza kasi ya maendeleo ya shirika hilo.
“Tusameheane tunapokoseana kwani tukishindwa kufanya hivyo hatutaweza kufanya kazi zetu vizuri,” alisema.