NEW YORK,MAREKANI

KUNDI la watu wanaomuunga mkono Rais Donald Trump wa Marekani limevamia jengo la serikali, “Capitol Hill” jijini Washington, ambako wabunge walikuwa wakihitimisha ushindi wa rais mteule Joe Biden katika sanduku la kura.

Zoezi hilo lilisitishwa kwa muda lakini kikao kimeendelea baada ya mambo kuwekwa sawa kwenye jengo hilo.

Kundi hilo lilivuka uzio wa polisi na kufurika kwenye roshani.Baadaye kundi hilo lilielekea kwenye vyumba vya Maseneti, Baraza la Kongresi na ofisi za wabunge kadhaa.

Vyombo vya habari vya Marekani vilisema kuwa mwanamke mmoja alipigwa risasi na baadaye kufariki. Mkuu wa polisi wa eneo hilo alisema kuwa maofisa kadhaa walijeruhiwa.

Meya wa jiji la Washington alitoa agizo la kukaa ndani majira ya usiku kwa jiji zima. Polisi wa kutuliza ghasia na vikosi vya Ulinzi vya Taifa vimepelekwa jijini humo kusaidia kuimarisha ulinzi.

Biden ameita tukio hilo kwamba ni ishara ya demokrasia ya Marekani kuwa hatarini. Biden alisema,Demokrasia inakabiliwa na mashambulizi yasiyowahi kutokea ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika nyakati za hivi karibuni.

“Hali hiyo inapaswa kuisha sasa.Natoa wito wa kundi hilo kuondoka na kuruhusu kazi ya demokrasia iendelee.”