NA KHAMISUU ABDALLAH

TASISI za serikali, Wizara na mashirika zimeombwa kushirikiana na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) katika kufanikisha ukusanyaji wa kodi za serikali ili kufikia malengo waliojiwekea.

Ombi hilo, lilitolewa na Meneja Uhusiano na Huduma kwa Walipa kodi wa bodi hiyo, Shaban Yahya Ramadhan, wakati akizungumza na wahasibu na maofisa mapato waliokuwepo katika taasisi mbali mbali za serikali na mashirika wanaoshughulikia mapato katika ofisini kwake Mazizini.

Alisema ushirikiano ndio njia pekee itakayowezesha bodi hiyo kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali. 

Aidha alisema ZRB haiwezi kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato bila kuwepo kwa taasisi ambazo zitaweza kuhakikisha zinasimamia ipasavyo kodi za serikali zinakusanywa kwa wakati, ili kuimarisha huduma mbalimbali za jamii.

Alisema ni ukweli usiopingika kuwa kuna tasisi nyingi za serikali haziwasilishi mapato yao katika bodi hiyo, jambo ambalo linarejesha nyuma kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.

Meneja Shaaban alisema tasisi za serikali nazo zina mapato hivyo zinawajibika kuhakikisha mapato hayo yanafika katika mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya kuiwezesha serikali kufikia mipango yake ya kimaendeleo.

Aidha alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021serikali imekadiria kukusanya shilingi 1,050 bilioni kutokana na vyanzo vya ndani ambapo kati ya makadirio hayo mapato ya kodi ni shilingi 921.3 bilino na mapato yasiyo ya kodi yanakadiriwa kufikia 128.7 bilioni.

Alibainisha kuwa TRA inakadiriwa kukusanya shilingi 383.5 bilioni na ZRB imekadiriwa kukusanya 516.7 huku wizara zikikadiriwa kukusanya shilingi bilioni 128.7 ikiwemo ada zinazotozwa na wizara mbalimbali za jumla ya shilingi bilioni 104.7.

Kwa upande wa gawio la faida inayotokana na mashirika ya serikali alisema ni shilingi bilioni 10.5, gawio kutokana na faida ya Benki kuu ni shilingi bilioni 13.5 huku ikitarajiwa kupokea bilioni 21.0 kama kodi ya mapato kwa wafanyakazi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano waliokuwepo Zanzibar.