NA RAMADHANI ALI MAELEZO
KAIMU Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dk. Ali Said, amewataka wahitimu wa stashahada ya Ukunga na Uuguzi ya chuo hicho kulinda maadili ya Kada hiyo watakapoanza kazi.
Dk. Ali alitoa ushauri huo katika Kampasi ya SUZA, Vuga wakati wanafunzi wa Idara ya Ukunga na Uuguzi wa Skuli hiyo walipoandaa sherehe za kuwakaribisha wanafunzi wapya wa Kada hiyo kwa mwaka 2020/2021.
Aliwaeleza wanafunzi waliohitimu mafunzo hayo na wanafunzi wapya kwamba Kada ya Uuguzi na Ukunga inahitaji uadilifu, nidhamu na uajibikaji wa hali ya juu kama ilivyoelekezwa na mwanzilishi wa kada hiyo duniani.
Mkuu wa Skuli hiyo Ali Said, aliwashauri wahitimu hao kutotosheka na elimu waliyopata bali waendelee kutafute nafasi za kujiendeleza zaidi kwani elimu haina mwisho.
Msaidizi Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za tiba ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakuga Zanzibar Prof. Amina Abdulkadi,r alieleza kuwa azma yake ya kuzalisha wauguzi wenye sifa imekamilika baada ya SUZA kuanzisha shahada ya kwanza katika Kada hiyo.
Aliwashauri wahitimu wa stashada ya Uuguzi na Ukunga waliomaliza kujiunga na Jumuiya za Kitaifa na Kimataifa, ili kupata uzoefu na kuleta mabadiliko na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha aliwakumbusha umuhimu hao kufanya tafiti, kuandika machapisho mbali mbali pamoja na kuwa wabunifu, ili kuiendeleza kada ya Uuguzi na Ukunga.
Katika risala ya Wanafunzi iliyosomwa na Asha Ali Khamis, walieleza mafanikio yaliyofikiwa katika Idara ya Uuguzi na Ukunga. Hata hivyo, walisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madarasa maalum ya wauguzi na wakunga na vifaa vya kisasa vya maabara ambazo zinawasumbua katika masomo yao.