MARA

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara, ameiagiza Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara kusitisha utupaji taka katika lililopo Mtaa wa Starehe baada ya kutoridhishwa na mazingira yake.

Waitara ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwa lengo la kukagua mazingira ya mji huo.

Akizungumza akiwa katika ziara hiyo alisema haridhishwi na uwepo wa dampo hilo katika eneo la makazi ya watu na kuuelekeza uongozi wa halmashauri hiyo kutenga eneo maalumu Magena nje kidogo ya mji kwa ajili ya kutupa taka. 

Alionesha kutoridhishwa na uwepo wa dampo hilo katikati ya makazi ya watu akisema linahatarisha afya za binadamu ambapo wakati wa mvua limekuwa likitiririsha uchafu kwenda kwenye makazi ya wananchi.

“Hapo kuna dampo na kuna taka zinatupwa ovyo karibu na makazi ya watu jambo hili ni hatari kwa afya watoto wanacheza pale sasa naagiza lifungwe tunapoanza mwaka mpya uchafu usitupwe tena hapa nasikia mmetenga eneo lenye ukubwa wa karibu ekari kumi sasa,” aliagiza.

Aidha, Waitara alimuelekeza Afisa Mazingira wa halmashauri ya mji huo, Erasto Mbunga kuhakikisha takataka zilizotupwa pembezoni mwa barabara zinaondolewa mara moja na kutupwa sehemu maalumu.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Naibu Waziri huyo, kubaini uwepo wa taka hizo akiwa njiani katika ziara yake mjini Tarime haraka na kupelekwa maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili hiyo.

Akitoa maoni Diwani kutoka halmashauri hiyo, Chacha Machugu alidai kuwa kuna changamoto ya uhaba wa magari ya kubebea taka akisema kuwa kwa sasa liko moja wakati lingine liko kwenye matengenezo hali inayosababisha ugumu katika kuzoa taka.

Pia Machugu aliomba Serikali iendeleze utaratibu wake wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira kwani kwa sasa wengi hawashiriki katika zoezi la kufanya usafi