NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAJASIRIAMALI wa kikundi cha ufugaji wa kuku wa kienyeji cha ‘Siri Yako’ kilichopo shehia ya Tumbe Magharibi wameiomba Serikali kuwapatia mkopo, ili waongeze uzalishaji wa mifugo yao.

Walisema kuwa, iwapo watapatiwa fedha wataweza kununua kuku wengi pamoja na kuimarisha eneo la kufugia, jambo ambalo liwasaidia kuzalisha na kupata kipato kitakachowasaidia kuwakwamua na maisha

duni.

Walieleza kuwa, kikundi chao ni wanaume watupu ambao walikaa pamoja na kutafakari kuanziasha mradi ambao utawapatia fedha za kuwasaidia kuendesha familia zao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Tumbe akinababa hao walisema, lengo la kuanzishwa ufugaji wa kuku ni kujikwamua na umasikini ingawa bado hawajafikia lengo  walilokusudia.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Msabah Haji Abeid alisema kuwa, ufugaji huo walianza Septemba mwaka 2020, ambapo walianza na kuku 20 waliotoa wenyewe binafsi.

Alieleza waliamua kufuga kuku wa kienyeji kutokana na kuwa wana bei kubwa, ingawa bado wana kiwango kidogo ambacho kitasababisha kuchelewesha mafanikio.

“Tunataka tupatiwe mkopo, ili kuku wawe wengi, hii itasaidia kuzalisha kwa wingi na ndipo tutaweza kujikwamua”, alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho Bakar Haji Abeid alisema, pia wanahitaji banda lililozungushwa uzio, ili kuku hao wasiende kuchumia mbali.

“Tutakapopata mtaji tutaweza kujenga banda kubwa lenye kiwango kinachokubalika na kuzungusha uzio, hii itasaidia pia kupungua kuibiwa”, alisema Katibu huyo.

Alieleza hadi sasa  bado hawajapata mafanikio kutokana na kuwa mradi wao bado ni mdogo lakini wanaamini kwamba watanufaika sana iwapo watakuwa na kuku wengi.

Nae Mjumbe wa kikundi hicho Mfaki Nassor aliiomba Serikali,  kuwapatia elimu, ili wafuge kitaalamu na sio kwa mazowea, kwani inapotokezea changamoto kwa sasa hawawezi kuitatua.

Nae Mjumbe Omar Msabah Haji alisema kuwa, kuku hao wamewajengea karibu na mashamba yao ya mpunga, ambapo muda mkubwa wanakuwepo hapo kuwashughulikia pamoja na kuwalinda.

Mratibu wa Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Pemba, Haji Khamis Haji alisema wanawawezesha wajasiriamali mbali mbali kwa kuwapatia mikopo na mafunzo, ingawa kikudi kilichokuwa hakijasajiliwa hakiwezi kupatiwa mkopo.

“Kwanza wakasajili kikundi chao kwa kufuata taratibu zinazotakiwa, kisha waje kuomba mkopo, sisi tutakwenda kukagua na ikiwa wametimiza vigezo na masharti tutawapatia, kwani Serikali imetoa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali”, alisema.

Alisema kuwa, katika wilaya ya Micheweni wameshatoa mikopo 181 kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana, ambapo jumla ya shilingi 152,000,000/= zimetolewa kwa vikundi na mtu mmoja mmoja.