Mwenyewe aridhia maamuzi

NA MWAJUMA JUMA

UMOJA wa klabu za soka Zanzibar umemuondoa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Zanzibar Kassim Ali, kutoendelea na nafasi hiyo ikiwa ni miezi miwili tu tangu kuchaguliwa kwake Novemba 14 mwaka jana.

Mwenyekiti huyo ameondolewa katika nafasi hiyo kwa kukabiliwa na tuhuma mbali mbali, ikiwemo kushindwa kutekeleza maagizo ya umoja huo waliyoyatoa Januari 10 mwaka huu na kuvujisha siri za maagizo hayo kabla ya kuyafikisha kwa wahusika kwa vipindi tofauti.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi za Shirikisho la Soka Zanzibar, Katibu wa timu ya Malindi Mohammed Masoud alisema maazimio ya maamuzi hayo yalitolewa katika kikao cha pamoja kilichofanyika Januari 17 mwaka huu, huko ukumbi wa Mafunzo Kilimani.

Alisema  katika kikao hicho wajumbe walitoa maazimio yao ambayo kwa bahati mbaya yalivuja kabla ya kufika kunakohusika kama ambavyo alitakiwa kufanya.

Hata hivyo alisema sio mara ya kwanza kufanya hilo na alishapewa onyo kwa makosa mbali mbali, ambayo yalikuwepo nyuma na baadae Bodi ya Ligi kushindwa kumtetea.

Alisema katika kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Sheha Khamis, kilikuwa na kazi kubwa baada ya kujitokeza wajumbe wote waliohudhuria kutokuwa na imani nae na kulazimika kupigwa kura za siri na zote zilimkataa.

Alifahamisha kwamba jumla ya klabu tisa zilishiriki kikao hicho na kutoa maamuzi hayo huku hatua zaidi zilifuatiliwa ili kupatikana Mwenyekiti mwengine.

Alifahamisha kwamba kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wa Bodi pamoja na klabu ambapo wajumbe wa bodi, hawakupiga kura na kati ya klabu 12 klabu tisa zilihudhuria.

Alizitaja klabu ambazo wajumbe wake walipiga kura ni Mafunzo, KVZ, Zimamoto, Chuoni, Polisi,  Malindi, Mlandege, KMKM na JKU huku klabu tatu zikiwemo Kipanga, Hard Rock na Black Sailor hazikuhudhuria.