NA KHAMISUU ABDALLAH

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watu wanane waliokamatwa katika eneo la Darajani Mnadani wakituhumiwa kuuza simu zinazosadikiwa kuwa za wizi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Mwembemadema.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Abdulkarim Jabir Suleiman (35) mkaazi wa Magomeni akiwa na simu 32, Ahmed Nassir Hamad (25) mkaazi wa Bububu akiwa na simu nane, Ibrahim Mshamu Mbwana (23) mkaazi wa Amani akiwa na Simu 10 na Kassim John Bundala (34) mkaazi wa Kwaboko akiwa na simu 24.

Wengine ni Mahmoud Juma Salum (40) mkaazi wa Fuoni akiwa na simu 14, Abdalla Makame Silima (22) mkaazi wa Mfenesini akiwa na simu nane, Zakaria Shija Zakaria (28) mkaazi wa Fuoni akiwa na simu tisa, Gharib Soud Mohammed (33) mkaazi wa Migombani akiwa na simu tatu na kijana aliyetambulika kwa jina moja la Yassir aliekimbia na kuacha simu 11.

Kamanda Awadh, alisema watuhumiwa wote hao walikamatwa Disemba 29 majira ya saa 7:30 mchana katika maeneo ya Darajani Mnadani wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Aidha alisema watuhumiwa wote hao walikamatwa katika maeneo hayo wakijishughulisha na biashara ya kuuza simu na kununua simu za wizi.

“Watuhumiwa hawa tuliwahoji kwa kina na tumegundua kwamba baadhi ya simu walizokuwa nazo hazina risiti ambazo waliuziwa na watu wanaoojihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu,” alisema.