ADDIS ABABA,ETHIOPIA

SHIRIKA  la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR linaendelea kuandikisha wakimbizi wapya katika mpaka wa Sudan na Ethiopia ambapo takriban wakimbizi 800 wamevuka kutoka eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuingia mashariki mwa Sudan.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic alisema tangu Novemba mwaka jana, zaidi ya wakimbizi 56,000 kutoka Ethiopia walikimbia machafuko na kuingia nchi jirani Sudan.

UNHCR ilisema wakimbizi wanaowasili wanafika na nguo tu walizovaa, wakiwa wamechoka na wakiwa dhaifu baada ya safari ya siku nyingi.

Asilimia 30 ya  wakimbizi wanatajwa kuwa chini ya umri wa miaka 18 na asilimia tano wana umri wa zaidi ya miaka 60.

Mahecic alisema kwamba kwa kushirikiana na serikali ya Sudan,UNHCR na kamisheni ya wakimbizi Sudan, COR wanaendelea kuhamisha wakimbizi kutoka kwenye maeneo ya mapokezi ambayo yamejaa hadi kwenye kambi zilizoko jimbo la Gedaref.

Aidha alisema mahitaji ya wakimbizi ni mengi na kwamba,Serikali ya Sudan inaendelea kuacha mipaka yake wazi kwa ajili ya wakimbizi lakini msaada zaidi unahitajika hususan kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji kwenye kambi na maeneo ya mapokezi.

Mapigano yanaripotiwa kuendelea katika mkoa wa Tigray, karibu miezi miwili sasa baada ya kuzuka kwa mapigano katika jimbo hilo linalotaka kujitenga.

Serikali ya Ethiopia inasisitiza kuwa hali ni shwari katika mkoa wa Tigray, lakini ni vigumu kuingia katika jimbo hilo Tigray.